2014-05-31 09:06:08

Lengeni mbali zaidi!


Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume hivi karibuni wamekuwa wakishiriki katika mkutano wao wa mwaka ili kujibu changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana nao kwa mara ya mwisho tarehe 29 Novemba 2013 na kutangaza nia yake ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani 2015.

Katika mkutano huu, wakuu wa Mashirika wameangalia mbali zaidi katika maisha na utume wa kitawa ndani ya Kanisa; maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ushiriki mkamilifu katika mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Majimboni pamoja na kuendelea kutuma Wamissionari katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Wakuu wa Mashirika wamepembua pamoja na mambo mengine umuhimu wa kuendeleza shughuli za kimissionari kwa njia ya ushuhuda unaofumbatwa katika unabii, karama ya Shirika pamoja na kuendelea kushikamana na Kanisa la Kiulimwengu. Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu "Kuuamsha ulimwengu. Watawa katika utume wa Kanisa leo".

Wakuu wa Mashirika wamehamasishana kuivalia njuga changamoto inayoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko ya kutoka huko "walikojificha" kwenye nyumba za kitawa, tayari kujimwaga uwanjani ili kuhamasisha ukuaji wa miito ya kitawa na kazi za kitume ndani ya Kanisa.

Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanataka kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayoadhimishwa mjini Vatican mwezi Oktoba, 2014. tafakari yao italenga zaidi katika kuonesha uhusiano wa dhati uliopo kati ya Familia na Maisha ya Kijumuiya katika Mashirika ya Kitawa!

Hapa Wakuu wa Mashirika wanasema, mambo si shwari sana, kunawaka moto huko Mashirikani, changamoto ya kuhakikisha kwamba, maisha ya kitawa yanaboreka zaidi kwa kuzingatia utu na kanuni msingi za maisha ya Kikristo! Mashirika ya kitawa hayana budi kujichunguza na kuangalia ni mambo yepi yanayowakosesha furaha wanashirika wake, ili kuyafanyia kazi, tayari kushiriki katika mchakato wa utangazaji wa Injili ya Furaha miongoni mwa watu wa mataifa!

Watawa wanapaswa kuwa makini zaidi katika maisha na utume wao kwa kutafuta na kuzingatia yale mambo msingi, ili wasije wakamezwa na malimwengu! Mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Ufukara na Useja ni mambo msingi katika kuonesha kipaji cha unabii kati ya watu kwa ajili ya watu! Haya ni mambo ambayo kamwe hayapaswi kufanyiwa mzaha, ndiyo maana Watawa wanahimizwa kulenga mbali zaidi kwa kutambua kwamba, wanaitwa na kutumwa kushiriki mambo matakatifu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu wanayohudumia.

Wakuu wa Mashirika wanasema, kuna haja ya kumwangalia Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro! Ni kiongozi anayeonesha fadhila ya unyenyekevu kwa kuzingatia mambo msingi; utu na heshima ya binadamu; ni kiongozi mwenye maneno machache, lakini matendo yake yanagusa sakafu ya mioyo ya watu wengi! Mwelekeo kama huu unaweza pia kuleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa kwa kukazia mambo msingi.

Wakuu wa Mashirika wanapaswa pia kutekeleza dhamana na utume wao kadiri ya sheria za Kanisa na zile za Mashirika yao, kwa kuwatembelea na kuwasikiliza na kuzungumza na watawa wa Mashirika yao. Dhamana hii ni muhimu sana katika kubadilishana mawazo, uzoefu na mang'amuzi ya maisha na utume wa Mashirika katika Kanisa. Wakuu wa Mashirika waoneshe ile fadhila ya udugu na ubaba kwa kutambua kwamba, cheo ni dhamana, lakini wao kwa pamoja ni sehemu muhimu sana ya Shirika inayounda Familia ya Mungu.

Wakuu wa Mashirika wanabainisha kwamba, kinzani na migogoro ndani ya familia ina athari kubwa katika maisha na utume wa watawa ndani ya Mashirika yao. Ikiwa kama wadau mbali mbali hawataweza kutunga sera makini pamoja na kutoa msaada unaohitajika katika familia, itakuwa ni vigumu sana kwa Kanisa pia kutekeleza dhamana na utume wake ulimwenguni. Kuna haja ya kuwa na sera makini zinazounga mkono tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kwa upande wake, Kanisa halina budi kujielekeza zaidi katika utume wa Familia.

Wakuu wa Mashirika wanasema, katika ulimwengu mamboleo, Kanisa lina dhamana kubwa ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kukazia umuhimu wa Sakramenti za Kanisa: Ndoa, Ubatizo, Kipaimara, Mpako wa wagonjwa. Katika ulimwengu wa utandawazi, sayansi na teknolojia watu wanataka uhuru usiokuwa na mipaka, lakini Kanisa liendelee kuwafunda watu umuhimu wa kuthaminiana na kuona ukweli wa mambo!

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.,
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican







All the contents on this site are copyrighted ©.