2014-05-31 10:15:57

Ametuacha vibaya!


Amepaa mbinguni na ameketi mkono wa kuume wa Mungu:

Siku arobaini baadaye ….. Mt. 1,23 – Mungu yu nasi leo tena tunasikia tamko hilo la Yesu mwenyewe.Maana yake nini? Hivyo tunaadhimisha leo uwepo wa Mungu kati yetu na uwepo wa Mungu kati yetu waoneshwa na kazi za watu wake wanaomtii Roho Mtakatifu.

I. Mdo 1,1-11
II. Efe. 1,17-23
III. Mt. 28,16-20

UTANGULIZI

Sherehe ya kanisa siku 40 baada ya sherehe ya Pasaka - kupaa mbinguni Bwana wetu Yesu Kristo. Mhubiri mmoja asema hakuna awezaye kukaa peke yake mke/mume ahitaji mke/mume mwema, mwalimu ahitaji wanafunzi wa kinyume chake nini?

Hivi pia kwa mkristo leo hii yupo Roho Mtakatifu na akiwepo utamu wa maisha ya kikristo huongezeka. Katika Mt. 1,23 tunaambiwa kuwa Mungu yu pamoja nasi.
Leo Yesu asema nipo pamoja nanyi. Sikukuu ya Kupaa siyo kumbukumbu ya Kristo kuondoka kati yetu bali kumbukumbu ya uwepo wa Kristo kati yetu. Uwepo huu unaoneshwa na kazi zifanywazo na watu wa Mungu wake ambao daima wanatii Roho mtakatifu.

Tunapoona habari ya Kupaa Bwana iko wazi - Yoh 3,13 - wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni yaani Mwana wa Adam - Efe 4,10 - naye aliyeshuka ndiye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote ili avijaze vitu vyote. Ebr. 4,14 – basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia mbinguni Yesu, Mwana wa Mungu, tuyashike tena maungamo yetu.

Na tukisoma alifufuka/kupaa - Yoh 20,17 Yesu akamwambia (Mariam) usinishike kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu. Lk 24,51 ikawa katika kuwabariki alijitenga nao akachukuliwa juu mbinguni.

Yesu alipaa mbinguni mwili na roho na tendo hilo limetokea siku ile ile ya ufufuko wake kadiri ya Wainjili - Mt, na Mk – ilitokea Galilaya mara moja na hivyo tu. Katika Lk, na Matendo - alipaa na hii ilifanyika siku 40 baada ya ufufuko na katika muda huo ametokea mitume mara kadhaa. Lakini lengo la waandishi siyo uhakika katika mandishi bali katika ujumbe wa tukio hilo kuu. Adhimisho la sikuku hii ya leo laonesha tu mwisho wa muda/wakati ambao Yesu bado alihusiana kwa macho na wanafunzi wake.

Tunachoambiwa ni kuwa atakuja tena siku ya mwisho - Yoh 21,22 Yesu akamwambia ikiwa nataka huyu akae hata nijapo imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi?
1 Kor 15,23 lakini kila mmoja mahali pake limbuko ni Kristo baada ya walio wake Kristo atakapokuja.

Hakika masomo yetu ya leo - liturjia yetu yahimiza ufuasi katika ukweli - kwamba maana halisi ya maisha ya kikristo ipo katika Kristo mwenyewe. Mitume wanahimizwa wakaze mwendo na kuongoa wengi wakibatizwa na kufundisha. Nguvu yao ni Kristo na wao wenyewe.

Yesu aliye na nguvu ya Baba anatoa uwezo huo huo kwa wafuasi wake.

I. Ufuasi ni mchakato ambao kila mwamini anaelimishwa na kuingizwa katika njia mpya/ni mchakato wa uinjilishaji.
Huu ndio mwili uliotolewa na jukumu kuu walilopewa wafuasi wakati wa kupaa Bwana - nao wakafanye aliyofanya Bwana - kuendeleza utume wake Bwana. Huu ni wosia wakati wa kupaa.

II. Katika kupaa kwake Bwana - upatikanaji wa nguvu kwao wote wamfuatao. Yeye atamani kubaki na watu wake ndio maana asema mimi nipo kati yenu. Hatuachi peke yetu. Yote asemayo yatuachia furaha, amani na maneno hayo bado yanabaki kati yetu kuwa na maana kubwa. Hata leo tunahitaji uongoi wake Kristo.

Ni sikuku ambayo sote tunaitwa kutambua kuwa yule Kristo tumwaminiye amepaa mbinguni na ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba, ametukuzwa na ana mamlaka yote na atakuja tena na ukuu na enzi.

Baada ya kusikia hayo yote ni upi ujumbe?

- Mdo 1,8- lakini mtapokea nguvu ya Roho atakayewashukia na mtakuwa mashahidi wangu Yerusalemu na katika nchi yote ya Yudea, Samaria na hata miisho yote ya dunia.

- Mt 28,19-20 – basi nendeni mkayafanye mataifa yote kuwa wafuasi mkiwabatiza kwa jina la Baba. Mkiwafundisha kushika yote niliyowaagiza. Na tazama nipo nanyi siku zote mpaka mwisho wa dunia.

- Mk 16,15-18 – akawaambia nendeni ulimwenguni kote kuleta uzima.
Yesu alitoa tamko la utume - tena wafanye kwa uaminifu mpaka atakapokuja. Aliwahakikishia mema ya Mungu katika utumishi wao.

Hili tamko la utume ni lipi? Ushuhuda katika kueneza habari njema mpaka miisho ya dunia katika mataifa yote na kutangaza kwa kila kiumbe. Hii habari ni habari njema ya ufalme wake bila kuwa na mipaka ya utaifa au ukabila.

Huu ndio ujumbe tena unaowekwa mbele yetu tunaposherehekea sikukuu ya Kupaa Bwana. Mimi naenda ili aje yule Roho. Ujumbe huo ni wa Bwana, ndiyo maana atuahidi Roho mtakatifu. Peke yetu tutashindwa.

Sherehe hii yathibitisha ukamilifu wa upendo wa Mungu. Mungu amekamilisha utume wake hapa duniani. Ametufundisha juu ya ufalme wake, ametuaminisha sisi watu wake tuendeleze hilo jukumu, anatutuma sisi tuende sasa ulimwenguni lakini pamoja na Roho wake. Hakika ni uaminifu mkubwa. Hii ndiyo changamoto - ikiwepo mbele yetu leo – nasi tuende tukahubiri hiyo habari njema.

Uwepo wa Kristo kati yetu ni ushuhuda wetu wa maisha ya kikristo. Tunaalikwa tuishi hapa duniani, yale ya mbinguni. Papa Paulo VI anasema - ulimwenguni unahitaji zaidi mashuhuda kuliko walimu. Lk. 24:48 - ninyi ni mashahidi wa mambo hayo.

Katika Waraka kwa Ebr. 10: 21-23 – tunasoma hivi: tunaye kuhani mkuu aliyewekwa juu ya nyumba ya Mungu. Kwa hiyo tujongee kwa mioyo minyofu na imani kamili, maana mioyo yetu imenyunyuziwa na kusafishwa dhamiri mbaya, na miili yetu imeogeshwa katika maji safi. Na tuyashikilie matumaini tunyoungama bila kusitasita, kwa maana yeye aliyetoa ahadi ni mwaminifu.

Imetayarishwa na Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.