Wanasiasa onesheni ukweli, uwazi na uaminifu kwa umma!
Askofu Felix Ajakaye wa Jimbo Katoliki Ekiti, Nigeria katika maadhimisho ya kumbu
kumbu ya miaka 10 tangu Kanisa la Parokia ya Fumbo la Utatu Mtakatifu lilipozinduliwa
katika Jimbo kuu la Abuja, amewataka Wakristo walioko kwenye uwanja wa kisiasa kushiriki
kikamilifu kwa kuonesha uaminifu na uwajibikaji katika kulinda na kutetea mafao ya
wengi, ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Nigeria.
Ushuhuda wa maisha
unapaswa kujionesha katika medani mbali mbali za maisha na kwa njia hii wanashiriki
kwa dhati kabisa katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu, changamoto kubwa katika
mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo na kwa namna ya pekee nchini Nigeria. Wakristo
wajipambanue kwa huduma makini, uadilifu, ukweli na uwazi katika kuwahudumia wananchi
wa Nigeria, ili kweli waweze kuwa ni mfano bora wa kuigwa na jirani zao wengine.
Askofu
Felix Ajakaye anasema, huu ndio ushuhuda wa imani katika matendo, inayoonesha mashiko
na mvuto kwa wananchi mbali mbali kwani watu wamechoka na maneno matupu yanayotolewa
kwa kiasi kikubwa na wanasiasa. Kwa bahati mbata tasnia ya siasa imeingiliwa na watu
wenye uchu wa mali, madaraka na sifa, kiasi cha kuwafanya watu wengi kuchukia mambo
ya kisiasa kwani wanaona siasa kuwa ni mchezo mchafu!
Hii inatokana na ukweli
kwamba, kuna watu wanavamia jukwaa la kisiasa kwa kutaka kujitajirisha wao na familia
zao badala ya kuwa ni huduma makini kwa jamii. Kutokana na dhana kama hii, Kanisa
halina budi kusimama kidete kuwaelimisha watu kuzingatia utawala bora; ukweli na uwazi;
ustawi na maendeleo ya wengi. Wanasiasa wajenge utamaduni wa kuwa watu wanaosimamia
na kutetea ukweli na uaminifu.
Ushuhuda huu unapaswa kuonekana kwa namna ya
pekee miongoni mwa wanasiasa Wakristo wanaoshirikisha karama na mapaji waliyokirimiwa
na Roho Mtakatifu kwa ajili ya wote. Askofu Felix Ajakaye anasema kuna haja kwa wanasiasa
kujielekeza zaidi na zaidi katika ukweli, uaminifu na uwajibikaji makini kwa watu
wao.