Nyanyaso za kijinsia zina madhara makubwa kwa watoto!
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema kwamba, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto
wadogo zinawaathiri sana watoto katika makuzi na malezi yao kwa sasa na kwa siku za
baadaye. Nyanyaso hizi zinagusa undani wa utu na heshima ya mwanadamu pamoja na utakatifu
wake, kwani mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Kanisa Katoliki nchini
Kenya katika mwongozo wake wa Mwaka 2011 linasema kwamba, linataka kusimamia na kuwalinda
watoto.
hayo yamebainishwa hivi karibuni na Padre Daniel Rono, Katibu mkuu
Msaidizi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya wakati akitoa hotuba kwa washiriki wa
semina ya ulinzi wa watoto wadogo iliyohudhuriwa na wakufunzi kutoka Majimbo yote
yanayounda Kanisa Katoliki nchini Kenya pamoja na wageni waalikwa kutoka Zimbabwe.
Padre
Rono anasema, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa na kuchangamotishwa
na Mama Kanisa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu tangu
pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika
kadiri ya mapenzi ya Mungu. Maisha ni matakatifu kwa sababu ni zawadi kubwa kutoka
kwa Mwenyezi Mungu ambayo binadamu amekabidhiwa kuilinda, kuitunza na kuiendeleza.
Kumbe, kuna haja kwa Kanisa kuwa macho zaidi dhidi ya nyanyaso kwa watoto wadogo!
Nyanyaso
zina madhara makubwa kwa watoto kwani zinaharibu taswira yao, uwezo wao wa kuhusiana
na watu wengine hata watakapokuwa watu wazima; wanaathirika katika masomo na makuzi
yao na matokeo yake wanaweza kujikita kwamba, wametumbukia katika matumizi haramu
ya dawa za kulevya na ukahaba, mwendelezo wa utumwa mamboleo kwa watu wa nyakati hizi.
Ni watu wanaweza kukumbwa na msongo wa mawazo na hatimaye, kutema zawadi ya maisha
kwa kujinyonga! Haya ni baadhi ya madhara ambayo anaweza kupata mtoto aliye nyanyaswa
kijinsia.
Kanisa nchini Kenya linataka kuhakikisha kwamba, watoto wanaopata
huduma mbali mbali katika taasisi zake wanakuwa salama, kwani wameumbwa na Mwenyezi
Mungu, ni wema na watakatifu; wanapendwa na kuthaminiwa na Mungu mwenyewe na kwamba,
wana fursa ya kuanzisha mchakato wa maisha yao kwa siku za usoni. Watoto wafundishwe
kuwatambua watu wanaoweza kuwanyanyasa kijinsia kwa njia za ulaghai.