2014-05-30 08:21:24

Makanisa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi


Mapambano dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi Barani Afrika yanakabiliana na changamoto mbali mbali zinazofumbatwa katika imani, mila, desturi na tamaduni za watu. RealAudioMP3

Haya ni mambo msingi yanapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa na viongozi wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, hasa kwa kuwajengea wanawake uwezo wa kujikinga na Ukimwi kwani wao ni wahanga wakuu wa maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Haya ni kati ya mambo yaliyojadiliwa na washiriki wa semina juu ya Ukimwi na Afya ya Uzazi, iliyofanyika hivi karibuni, Jijini Arusha, Tanzania, kwa kudhaminiwa na Chama cha Wanawake Wakristo Duniani, YWCA ambacho ni mwanachama wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Wajumbe katika mkutano huu wamepembua kwa kina na mapana kuhusu mchango wa Makanisa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi pamoja na mikakati iliyopo inayopania kuwajengea wanawake uwezo wa kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Wajumbe wanasema kwamba, kuna haja kwa Makanisa kuhakikisha kwamba, yanawajengea wanawake uwezo wa kutambua imani, mila na desturi njema za kutambua mambo yanayoweza kuwaongezea maisha badala ya kukumbatia imani, mila na desturi zinazowapeleka kwenye kifo. Wanawake watambue kwamba, wanakabiliwa na uwezekano wa kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi, wasipojikita katika maadili mema na uaminifu katika maisha yao ya ndoa. Wanawake wawe makini katika kujenga na kudumisha mahusiano yao ndani ya ndoa na maisha ya kifamilia, kwani ugonjwa wa Ukimwi umesababisha majanga makubwa kwa familia nyingi Barani Afrika.

Wajumbe katika mkutano wao Jijini Arusha, wanasema kwamba, kuna haja kwa viongozi wa Makanisa kujenga utamaduni wa majadiliano na ushauri nasaha ili kupambana na maambukizi ya Ukimwi katika maeneo yao. Ili kweli viongozi hawa waweze kutekeleza majukumu yao barabara, wanapaswa kunolewa na wataalam pamoja na wadau wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, ili kujipatia ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kupanga sera na mikakati makini katika mchakato wa mapambano dhidi ya Ukimwi.

Vituo vya kutunza na kulelea watoto yatima vimekuwa na mafao makubwa kwa watoto hao katika malezi na makuzi yao. Viongozi wa Makanisa wajifunze kuwasikiliza kwa utulivu na umakini mkubwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, ili kuondokana na tabia ya unyanyapaa unaokwamisha mchakato wa mapambano dhidi ya Ukimwi.

Ikumbukwe kwamba, Ukimwi si ugonjwa wa laana, kwani haubagui wala hauchagui. Watu wajengewe utamaduni wa kuheshimu na kuthamini Injili ya Uhai, ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwalinda, kuwatunza na kuwapenda wenzi wao wa ndoa, ili kamwe wasitumbukie katika maambukizi ya Ukimwi.








All the contents on this site are copyrighted ©.