Kamati kuu ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM,
imehitimisha safari yake ya kikazi mjini Vatican iliyoanza tangu tarehe 20 hadi tarehe
28 Mei 2014 kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu maisha na
utume wa Kanisa Amerika ya Kusini.
Katika mazungumzo na Baba Mtakatifu, Kamati
kuu ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, linasema kuna
haja ya kuendelea kuhamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusoma, kutafakari
na kumwilisha Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, Injili ya Furaha,
"Evangelii Gaudium" huko Amerika ya Kusini.
Imekuwa ni fursa kwa viongozi
hawa kumshirikisha Baba Mtakatifu Francisko yale yatakayojadiliwa na Maaskofu katika
kongamano lao la mwaka, kuhusu familia linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 4 hadi
tarehe 9 Agosti 2014. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuangalia changamoto zilizopo kwa
sasa anasema, pengine kuna haja ya kuadhimisha tena Sinodi Maalum kwa ajili ya Maaskofu
wa Amerika ya Kusini, kama Kanisa lilivyofanya kwa Maaskofu Katoliki Barani Afrika,
Sinodi iliyoitishwa kwanza kabisa na Mtakatifu Yohane Paulo II na kuridhiwa na Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI.
Kamati kuu ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu
Katoliki Amerika ya Kusini na Caraibi, limepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na
viongozi wakuu mjini Vatican pamoja na kutembelea baadhi ya Mabaraza ya Kipapa kuhusu
masuala ya: Mafundisho tanzu ya Kanisa, Utamaduni, Familia, Mawasiliano, Uinjilishaji
Mpya pamoja na Sinodi za Maaskofu. Viongozi hawa walibahatika kuzungumza pia na Tume
ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini pamoja na Mabalozi kutoka Amerika ya Kusini
wanaoziwakilisha nchi zao mjini Vatican ambao wamekabidhiwa hati kuhusu hali ya wakimbizi
huko Amerika ya Kusini!