2014-05-29 07:42:00

Papa Francisko kuwasha moto wa Injili mjini Roma!


Chama cha Kitume cha Uamsho wa Kikristo katika mkutano wake wa kitaifa uliohitimishwa hivi karibuni, kinasema, kimepokea kwa mikono miwili taarifa za uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kongamano lake la Kitaifa litakaloadhimishwa hapo tarehe 1- hadi 2 Juni 2014 kwenye Uwanja wa Michezo wa Olympic, mjini Roma. RealAudioMP3
Hii itakuwa ni Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni kwa Mwaka 2014. Kongamano hili litaongozwa na kauli mbiu “Tubuni! Aminini! Mtampokea Roho Mtakatifu. Kwa ajili ya Kanisa katika mwelekeo wa Kimissionari”.

Chama cha Kitume cha Uamsho wa Kikristo; waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wameanza kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya Maadhimisho ya Tukio hili la kihistoria linalojipambanua kwa kuwa ni fursa ya Sala na Uinjilishaji, kama sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa changamoto zinazoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa. Wakristo wanahimizwa kutoka huko “walikojificha” ili kutangaza, kushuhudia na kuwaonjesha jirani zao Injili ya Furaha.

Uwepo wa Baba Mtakatifu katika kongamano hili ni tukio la kihistoria kwa Chama cha Kitume cha Uamsho, kinachoonesha utashi na jitihada za Chama hiki kutaka kuunga mkono juhudi na mikakati ya kichungaji inayoendelea kuainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Kanisa halina budi kujikita katika huduma kwa walimwengu.

Kwa mara ya kwanza Papa Francisko ataingia kwenye Uwanja wa michezo wa Olympic ulioko Roma, ili kukutana na kuzungumza na wanachama wa Uhamsho wa Kikristo wapatao 50, 000 kutoka ndani na nje ya Italia. Ni kongamano ambalo litawashirisha baadhi ya viongozi waandamizi kutoka Vatican na wanachama mashuhuri wa chama cha Uhamsho kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Akizungumzia kuhusu tukio hili, Bwana Salvatore Martinez, Rais wa Chama cha Kitume cha Uamsho wa Kikristo anapenda kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kukubali mwaliko wao na kuamua kushiriki. Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko: Injili ya Furaha, waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kuonja ile Injili ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Yesu Kristo; kutambua na kung’amua utamu na uzuri wa kusali kama Jumuiya; kusikia ile nguvu ya ndani inayowasukuma waamini kujitosa kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Ibada ya Kuabudu, Sala ya Shukrani na Kusifu na neema ya Mungu inavyotenda kazi kwa Watu wa Mungu.

Bwana Salvatore anasema haya ni mambo msingi yanayowapambanua wanachama wa Chama cha Uamsho wa Kikristo katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa Katoliki; chama ambacho kwa sasa kinatimiza miaka 45 tangu kilipoanzishwa. Baba Mtakatifu Francisko anawafahamu fika kwani alikuwa ni mlezi wa Chama hiki alipokuwa bado nchini Argentina.

Hiki ni kipindi cha Uinjilishaji Mpya, mwaliko kwa waamini kutoka kifua mbele, kumshuhudia Kristo katika uhalisia wa maisha yao! Huu utakuwa ni mwanzo tu, lakini shughuli yenyewe itafanyika rasmi wakati wa Mkesha wa Siku kuu ya Petentekoste, Siku ya kuzaliwa kwa Kanisa, Siku ya Waamini Walei ndani ya Kanisa.








All the contents on this site are copyrighted ©.