Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon linakitaka Kikundi cha Boko Haram kilichowateka
Mapadre wawili na mtawa mmoja kuwaachilia mara moja ili waweze kuendelea na utume
wao miongoni mwa wananchi wa Cameroon. Itakumbukwa kwamba, Wamissionari hawa walitekwa
nyara nchini Cameroon hapo tarehe 5 Aprili 2014 na hadi sasa hawajulikani mahali walipo!
Ombo
hili limetolewa hivi karibuni na Kardinali Christian Tumi, Askofu mstaafu wa Jimbo
kuu la Doula nchini Cameroon. Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram kinausishwa na vitendo
vya utekaji wa watu nyara, Kaskazini mwa Afrika. Wakati ambapo Jumuiya ya Kimataifa
inasema hakuna sababu ya kufanya majadiliano ya magaidi wa Boko Haram bali ni kuendelea
kula nao sahani moja hadi kieleweke, lakini baadhi ya viongozi wa Serikali ya Cameroon
kama ilivyokuwa hata Nchini Nigeria wanasema, kuna haja ya kufanya majadiliano, ili
mateka waweze kuachiliwa huru na pia kudumisha utulivu.
Rais Paul Biya wa Cameroon,
hivi karibuni alipokuwa anashiriki mkutano dhidi ya vitendo vya Boko Haram Kaskazini
mwa Afrika, uliokuwa umeitishwa na Rais Francois Hollande wa Ufaransa alitangaza vita
dhidi ya vitendo vya kigaidi nchini mwake. Kanisa nchini Cameroon linasema nguvu yake
inajikita katika majadiliano kwani hawana silaha ya kupambana na magaidi. Hii ni changamoto
kwa Serikali kujikita katika utekelezaji wa mikakati endelevu ya ulinzi na usalama
wa raia na mali zao!