Taarifa ya Shirika la Kazi Duniani, ILO kwa Mwaka 2014 inaonesha kwamba, katika kipindi
cha miaka mitano ijayo, watu millioni 213 wataingia katika soko la ajira duniani na
kati yao kuna watu millioni mia mbili ni wale wanaotoka katika Nchi zinazoendelea
duniani.
Hapa kuna changamoto kubwa ya kuhakikisha kwamba, kunafanyika maboresho
katika maeneo ya kazi pamoja na kuwapatia wafanyakazi maisha bora zaidi. Katika nchi
zinazoibukia kwenye masuala ya kiuchumi kuna zaidi ya watu millioni 839 walioajiriwa
lakini wanaishi kwa dolla moja ya kimarekani kwa siku!
Shirika la Kazi Duniani
katika taarifa yake inayoangalia uchumi wa Nchi zinazoendelea duniani inaonesha kwamba,
kuna idadi kubwa ya vijana ambao hawana fursa ya ajira kwa asilimia 12% ikilinganishwa
na watu wazima. Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya kati ni kati ya maeneo ambayo
yamekumbwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa fursa za ajira duniani, kwani takwimu zinaonesha
kwamba, kati ya vijana watatu mmoja hana fursa ya kupata ajira.
Kwa bahati
mbaya wasichana wameathirika zaidi, kwani wasichana wasiokuwa na ajira katika eneo
hili ni asilimia 45%. Shirika la Kazi Duniani linasema kwamba, maboresho katika ubora
wa kazi unaweza kusaidia kupungua tofauti kubwa za fursa za ajira zinazojitokeza kwa
sasa.
Sheria za kazi hazina budi kuzingatiwa pamoja na kuendelea kuunga mkono
sera zinazosaidia kutengeneza fursa za ajira pamoja na kuwapatia wafanyakazi maisha
bora zaidi kama motisha katika uzalishaji na tija anasema Guy Ryder, Mkurugenzi mkuu
wa Shirika la Kazi Duniani. Fursa bora za ajira ni nyenzo muhimu sana katika mapambano
dhidi ya umaskini duniani. Kiwango cha chini cha mshahara ni jambo ambalo limeendelea
kupiganiwa na wafanyakazi sehemu mbali mbali duniani ili kuondokana na ubaguzi unaofanywa
hata katika viwango vya mshahara.
Shirika la Kazi Duniani linasema, kuna haja
kwa Nchi changa duniani kujifunga kibwebwe kupambana kufa na kupona na kazi za suluba
zinazowaingizia wahusika faida ya kiasi cha dolla za kimarekani millioni 150, lakini
inaacha madonda makubwa katika maisha ya wafanyakazi na familia zao. Takwimu zinaonesha
kwamba, kuna zaidi ya watu millioni 21 wanaofanya kazi za suluba sehemu mbali mbali
duniani. Hapa wasichana na wanawake wanaotumbukizwa kwenye biashara haramu ya ngono
ambayo faida yake inakadiriwa kufikia dolla billioni 99. Udhalilishaji wa kijinsia
ni kati ya changamoto kubwa kwenye sekta ya kazi na ajira duniani. Dhuluma hii inawakumba
hata watu wanaofanya kazi majumbani, kwenye sekta ya kilimo na uvuvi.
Shirika
la Kazi Duniani linaonesha kwamba, Bara la Asia linaongoza kwa biashara ya ngono duniani
kwa kuwa na watu zaidi ya millioni kumi na mbili, lakini pia linaongoza kwa kupata
faida kubwa katika masuala ya uchumi kwa kuwa na kiasi cha dolla za kimarekani billioni
52 za Kimarekani kwa mwaka. Takwimu zinaonesha kwamba, faida kwa watu binafsi kutoka
katika Nchi zilizoendelea zaidi duniani ni sawa na dolla za kimarekani 35, 000 kwa
kila mtu!