Je kustaafu kwa Papa Benedikto XV1, kunaweza kujenga utamaduni wa Mapapa kustaafu
?
Baba Mtakatifu Francisko , Jumatatu akiwa njiani kurejea Roma , alijibu maswali yote
11 yaliyoulizwa na waandishi wa habari. Kati ya maswali hayo ni iwapo kujiuzuru kwa
Papa Benedikto XV1, kunaweza kujenga utamaduni kwa Kanisa kwa Mapapa kustaafu wakifikia
umri fulani . Katika maelezo yake Papa Francisko alisema, ni wazi pia yeye angependa
kustaafu mapema kama mtangulizi wake Benedict XVI, badala ya kutawala maisha yake
yote, na kuongeza inawezekana dhana ya " Papa kustaafu " usoni inaweza kuwa jambo
la kawaida katika kanisa. Hata hivyo, amesema, yeye mpaka sasa ataendelea kulitumia
Kanisa kwa kadri Mungu anavyomjalia kiafya .Na anaweza kuachia ngazi iwapo afya yake
haitamruhusu kuendelea kuliongoza kundi la Mungu la waamini wa Kanisa Katoliki wapatao
bilioni 1.2 . Na kwamba kustaafu kwa Papa Benedikto XV1, isichukuliwe kama ni hatua
ya kushangaza, lakini kama kufungua mlango kwa Mapapa kustaafu. Papa Francisko
mwenye umri wa miaka 77 aliwaambia wanahabari, akitafakari hali halisi kwamba, kwa
sasa watu wengi wanaishi hadi umri mkubwa , na hii inaonyesha uwezekano kwa siku
zijazo, Mapapa kujiuzuru kutokana na umri mkubwa na hasa sababu za kiafya . Lakini
hili hakuna mwenye kujua kwa sababu afya ya Mtu ni kudra ya Mungu. Kujiuzuru kwa
hiari kwa Papa Benedikto XV1, Mwezi Februari mwaka jana, kuliandika historia mpya
ya Papa kujiuzuru, tangu Zama za Nyakati za Kati. . Salaam kwa Marais
Baba Mtakatifu pamoja na kujibu maswali ya waandishi wa habari, akisafiri kwa aina
ya ndege B777 el Al, kuelekea Roma, pia alituma salaam zake za Matashi mema kwa kila
Rais wa nchi ambako ndege yake ilipita. Akipita katika anga la Nchi ya Cyprus,
alipeleka salaam zake kwa Mheshimiwa Rais Nicos Anastasiades Rais wa Jamhuri ya
CYPRUS, na Rais Karolos Papoulias wa Ugriki, akisema, kwa mara ingine tena natoa
salaam zangu kwako na kwa wananchi wa Cyprus, wakati ninaporejea Rome tokea Nchi
Takatifu . Naomba Bwana, awabariki kila mmoja wenu kwa neema na amani na furaha .
Na
pia ndege ya Papa ilipita katika anga la Albania, na kutoa salaam zake kwa Rais Bujar
Nishani Rais wa Jamhuri ya ALBANIA , na kwa Mheshimiwa Rais Giorgio Napolitano
wa Italia, akisema, anarudi nchini Italia baada ya kukamilisha hija yake katika Nchi
Takatifu, ambako alikwenda kuhamasisha njia ya amani na mapatano baina ya watu na
dini. Na sasa kwake yeye Rais Napolitano na wananchi wa Italia, anamtolea Mungu ombi
maalum, kwa manufaa ya taifa zima la Italia. Na Rais Napolitano mara alijibu
salaam za Papa kwa kuonyesha matumaini yake kwamba, mwaliko wa kihistoria wa Papa
kwa Marais wa Israel na Palestina kukutana Vatican, kunatoa matumaini mapya
utulivu na amani katika mtazamo wa kuanza kwa mazungumzo ya amani kisiasa na kati
ya Wakristo, Wayahudi na Waislamu. Rais wa Jamhuri ya Italia, Giorgio Napolitano,
katika telegram yake kwa Papa ameiita ziara ya Papa katika nchi Takatifu kuwa ya
kukumbukwa na kugusa mioyo ya wale wote wanaopenda amani na utulivu duniani. Papa
alitua katika uwanja wa Ciampino (Rome) Jumatatu usiku na kurejea Vatican salama salimini.