2014-05-28 08:21:22

Hija ya Papa Francisko alama ya matumaini ya umoja wa Kanisa


Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema mkutano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, mwishoni mwa juma, ni tukio la kihistoria katika kukuza na kuendeleza ari zaidi katika majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Makanisa.

Mkutano wa viongozi hawa wakuu wa Makanisa uliofanyika mjini Yerusalemu Jumapili tarehe 25 Mei 2014 kwa kushirikisha mang'amuzi na vipaumbele vyao ni hija ya maisha ya kiekumene kuelekea katika ujenzi wa misingi ya haki na amani! Viongozi wa Makanisa katika tamko lao la pamoja wanakiri kwamba, wako katika hija ya umoja wa Kanisa unaoongozwa na Roho Mtakatifu katika umoja unaonesha tofauti za kweli. Haya ni mambo msingi yaliyojadiliwa pia katika mkutano wa kumi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni huko Korea ya Kusini.

Dr. Tveit anasema, mkutano wa viongozi hawa wa Makanisa umekuwa na maana kubwa kwa wao kukutana, kuzungumza na kusali mjini Yerusalemu kwenye Kaburi Takatifu, chemchemi ya imani ya Kanisa. Kwa hakika anasema Dr. Tveit, waamini na wananchi wanaoishi huko Mashariki ya Kati wameongezewa matumaini mapya katika hija ya maisha yao ya kiimani pamoja na kuendeleza mchakato wa amani na utulivu huko Mashariki ya Kati.

Sala na mkutano wa viongozi hawa ni changamoto kwa Makanisa kuendeleza mchakato wa haki na amani kwa watu wanaoishi huko Mashariki ya Kati pamoja na kuendelea kuimarisha maisha na utume wa Kanisa. Majadiliano ya kidini na waamini wa dini nyingine yamepewa mkazo wa pekee katika tamko la viongozi hawa wa Makanisa, lakini majadiliano ya kidini yana uzito wa pekee huko Mashariki ya Kati kutokana na kinzani za muda mrefu ambazo zimesababisha maafa makubwa, kiasi kwamba, baadhi ya Wakristo wanalazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na madhulumu ya kidini.

Dr. Olav Tveit anasema hija ya Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu kama kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana na kusali pamoja na patriaki Anathegoras wa Yerusalemu imekuwa ni alama ya matumaini na umoja kwa Makanisa yote ulimwenguni!







All the contents on this site are copyrighted ©.