2014-05-27 08:12:13

Watoto zaidi ya 500, 000 wanakabiliwa na baa la njaa nchini Somalia!


Mashirika ya misaada kimataifa pamoja na wadau mbali mbali wanaoendelea kutoa huduma nchini Somalia wanasema kwamba, kuna watoto zaidi ya laki tano ambao wako hatarini kukumbwa na maafa kutokana na baa la njaa, ikiwa kama hatua madhubuti hazitaweza kuchukuliwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuongeza bidii zaidi katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo mkali ambao unatishia maisha ya mamillioni ya watu duniani. Ni jukumu la Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, watu wanakuwa na uhakika wa usalama wa chakula. Hii ni kati ya changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Kunako mwaka 2011 Somalia ilikumbwa na ukame wa kutisha, kiasi kwamba, watu millioni 13 kutoka Pembe ya Afrika waliathirika vibaya sana. Umoja wa Mataifa unaonesha kwamba, kati ya mwaka 2011 - 2012, kuna watu 260, 000 wengi wao wakiwa ni watoto wamefariki kwa baa la njaa nchini Somalia. Baa la njaa linaanza kuinyemelea tena Somalia.







All the contents on this site are copyrighted ©.