Baba Mtakatifu Francisko baada ya kurejea mjini Vatican ili kuendelea na maisha na
utume wake kama kawaida, mapema asubuhi siku ya Jumanne, tarehe 27 Mei 2014 amekwenda
kutembelea Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma, kumshukuru Bikira
Maria kwa ulinzi na maombezi yake wakati wa hija yake ya kitume Nchi Takatifu.
Baba
Mtakatifu ameyaweka matunda yatakayopatikana baada ya hija hii ya kitume chini ya
ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria. Baada ya kuwasili, amepokelewa na viongozi wa
Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu na kusali kwa kitambo na baadaye kuweka shada la maua
kwenye Sanamu ya Bikira Maria.
Baba Mtakatifu amesalimiana na mahujaji pamoja
na waamini waliokuwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria huku akionesha furaha kubwa
moyoni mwake kwa kuhitimisha hija ya kichungaji iliyomwezesha kutembelea maeneo matakatifu
na kukutana na waamini wa dini mbali mbali kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa majadiliano
ya kidini na kiekumene, ili kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano
kati ya watu!
Hii ni mara ya tisa kwa Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi
cha mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kutembelea Kanisa
kuu la Bikira Maria mkuu!