2014-05-26 08:35:11

Maisha yenu yapambwe kwa utumishi adilifu!


Mpendwa msikiliziaji wa Kipindi chetu pendevu cha Kanisa la Nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo! Karibu katika mwendelezo wa mada yetu ‘maisha baada ya Pasaka’. Lengo letu ni kukumbushana, sisi kama Wakristo tuishi vipi upasaka wetu. RealAudioMP3

Kipindi kilichopita tulisema kwamba, maisha yetu ya kipasaka yaongozwe na matendo mawili makuu ya Kristo. Tendo la kuweka Ekaristi, ambapo tunamtazama Kristo aliyejisadaka, aliyejimega kwa ajili yetu na akaagiza tufanye vile vile kwa kumkumbuka yeye, na tendo la kuwaosha miguu wanafunzi wake, napo pia anaagiza akisema, nimewapeni mfano, ili ninyi nanyi mfanye vilevile. Kipindi kilichopita tulitafakari zaidi Uekaristi wetu katika familia (hasa wazazi) na katika mazingira yetu ya kazi.

Tunakazia maarifa kusema, sisi wakristo ni wabebakristo-wachukuakristo. Hivyo sote tuna wito wa pamoja kama wa-Kristo, kumdhihirisha Kristo huyo kwa watu nyakati zote. Kumchukua Kristo na kumpeleka katika mazingira ya maisha yetu ya kila siku. Neno kuu ni hili, tuwe tayari kujitoa sadaka kwa ajili ya wenzetu. Tuwe tayari kujimega ili kuchangia hali njema ya mwanadamu. Ni hivyo tu, tutamtambulisha na kumuenzi Kristo Yesu aliye sadaya ya wokovu wetu. Na wakati huohuo tufanyapo hivyo, sisi hatuwi tu Wakristo, bali tunakuwa nasi sadaka kwa ajili ya wokovu wa wengine.

Leo tuendelee na tafakari yetu kwa kutazama sehemu ile ya pili, yaani tendo la kuwaosha miguu wanafunzi wake. Ili ujumbe ufike kikamilifu, tuchukue maana ile mmoja tu ya kawaida yaani, katika tendo lile, kristo bwana anawafundisha wanafunzi wake utumishi mnyenyekevu. Watumikiane kwa upendo, wasaidiane, wainuane, watakasane, wanyenyekeane. Ni kwa njia hiyo tu wataweza kueneza vema ujumbe wa Injili.

Ndiyo maana anawapa swali zito sana akisema “"Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni?” (Yoh 13:12). Anaendelea kusema “Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni” (Yoh. 13:15). Sisi nasi tunataka maisha yetu ya kipasaka, yapambwe na Utumishi mwema na mnyenyekevu. Hatuwezi kuwa wainjilishaji kama hatupo tayari kutumikiana. Tutumikie kama Yesu alivyotufundisha.

Utumishi wetu unalenga kuwagusa wanadamu wote katika hali mbalimbali. Lengo la kufanya hivyo ni kumfanya Kristo aendelee kujulikana kwa watu na Injili yake imwilike katika maisha ya kila siku. Huduma yetu kwa watu hatusemi iwafanye watu kuwa Wakristo, hapana! Ila tunataka joto la upendo wa Kristo, liwaguse na kuwafariji wote.

Mambo yanayosaliti utumishi wetu:
Mpendwa msikikilizaji, kwa uchache tuyaangazie baadhi ya mambo yanaweza kufisha utumishi wetu na hivyo kupelekea kutokuwa mabalozi wa kweli wa Kristo Bwana aliyekuja kutumikia na sio kutumikiwa. Tukumbuke aliposema, nimewapeni mfano, ili ninyi nanyi mtende vivyo hivyo.

Kupenda ajira kuliko utumishi
Katika mazingira yetu ya kila siku, tunajikuta katika hali ambayo wengi tunatafuta ajira. Baadhi yetu wanabahatika kuajiriwa na wengine bado wanaendelea kutafuta. Na wakati wa kutafuta ajira, kila mmoja anajawa na hamu ya kupata kazi ya kufanya. Anafuata masharti yote hata kama ni magumu ali mradi apate ile ajira. Ajabu sasa, mtu akipata tu ajira, haoneshi tena moyo na moto wa kuichangamkia huduma kwa watu. Katika kazi yako, na ajira hiyo uwaone watu, tumikia watu kwa unyenyekevu wote.

Hukuajiriwa tu kwa ajili yako, ni kwa ajili ya huduma. Na tunaomba kukumbusha hapa, ajira yako, ni uwanja mpana zaidi wa kutangaza upendo wa mungu. Sasa kuna wale wenye bahati mbaya kubwa, wanaotumia ajira zao kama ndio kitu cha kuwanyanyasa na kuwadharau wengine.

Tukiyakuta mazingira kama hayo katika familia, tuaona baba kabla hajapata ajira alikuwa mtulivu, mwenye mshikamano na familia yake. Lakini mara tu alipopata ajira, ameanza kuwa jeuri, hatulii nyumbani, warsha kila baada ya nusu saa, anadharau mke wake na majirani, haendi kanisani tena nk. Mama naye kabla ya kupata ajira au kibarua alikuwa mama mwema, mke mwema, msikivu na mnyenyekevu. Lakini baada ya kupata kazi, anasahau familia yake. Nyumbani hafanyi kazi ya mama tena. Lugha za jeuri na matusi-mkuki zinaanza, kisa?? Ameajiriwa siku hizi, naye anashika hela yake, yupo huru!!! Ndugu, kazi yako isikunyang’anye utu wato!! Ajira yako ikuunganishe zaidi na wanadamu wenzako, na Mungu pia. Huo ndiyo mfano aliotuachia Yesu.

Ubaguzi na upendeleo

Jambo la pili linalosaliti utumishi wetu ni dhana ya ubaguzi na upendeleo inayoendelea kutamadunishwa katika mazingira yetu ya kila siku. Tukumbuke kuwa upendeleo sio upendo. Upendeleo hufukia haki. Jinsi Mungu wetu anavyowaangazia jua lake watu wabaya kwa wema, wenye haki na wasio haki, Kristo naye aliwahubiria neno lake watu wote. Na sisi ametutuma kwa watu wote wa mataifa yote. Ni aibu sana kama Mkristo katika hudumia anakuwa mbaguzi na mwenye upendeleo. Katika mahali pa kazi kama msimamizi, unalundika ndugu zako tu na marafiki zako, hata kama hawana uadilifu wala viwango vya kazi, hapo unaharibu utumishi.

Kama tutawabagua wengine bila sababu halali, hapo tunaharibu utumishi. Leo hii ofisi zetu nyingi zimepooza na kuudhi watu, kwa sababu ya ubaguzi na upendeleo. Yesu aliwaosha miguu wote waliokuwako pale karamuni, hata wale wabishi. Utumishi mwema na mnyenyekevu hauna ubaguzi wala upendeleo, bali umejaa upendo wa Yesu.

Kukosa uadilifu katika kazi

Uadilifu ni tunu msingi katika kazi, inayoyengwa katika dhamiri safi, imani kwa Mungu na uwajibikaji. Leo wengi tunashindwa kufanya kazi kiadilifu; utamaduni wa uhovyohovyo na roho ya bora liende, ndiyo vinatawala kazi zetu, hasa kazi za ajira, utumishi wa umma. Kukosa uadilifu kunajionesha zaidi katika roho ya tamaa ya mali, kutojali muda wa kazi, kutojali watu tunaowahudumia, kuwa na madai makubwa mno ya mishahara yasiyotazama wanyonge, roho ya ubadhilifu wa mali ya umma bila kujali maslahi ya wote, roho ya uwongo-unganishi katika kazi na mambo kama hayo, yanatufanya tusimwakilishe Kristo katika utumishi wetu. Mtumishi mwema na mwaminifu, hujali ubora wa huduma, huheshimu muda, huheshimu watu na mali ya mafaa kwa wote, na zaidi ya yote, humwona Kristo ndani ya watu wote!!

Utumishi wenye hila/ajenda za siri

Mpendwa msikilizaji, mara nyingi, tumeathirika na roho ya kutafuata faida binafsi katika mambo yote. Jambo hili linaharibu kabisa hata maana ya matendo mema tunayoyatenda. Hii roho ya kutafuta faida binafsi ndiyo inayotupelekea kwenye mitaala ya rushwa, na utamaduni wa ‘kitu kidogo’!! Katika hali hiyo, yule asiyeweza kutoa kitu kidogo hatahudumiwa, na atakufa na shida zake hivyohivyo. Utumishi wa kweli humlenga mtu kama mtu, na huelekezwa kwake huyo atumikiwaye bila kutegemea kupata chochote kutoka kwake.

Hila katika utumishi tunaweza kuiona wazi katika mifano ifuatayo:- Wizi: kuna watu wamejizoesha hivi, katika kazi yoyote lazima aibe tu, walao hata kidogo tu!! Hiyo ni hila. Mwalimu, askari, muuguzi nk, amejizoesha kupokea rushwa tu, hata kama ni ya pera moja. Huwa inakuwaje pale ambapo, baba unajitolea kusomesha yatima, halafu mwisho wa siku huyo yatima anakuwa mke wako. Sasa ulikuwa unamsomesha au ulikuwa na ajenda ya ten parsenti? Huo ndio utumishi wenye ajenda zilizofichika. Yesu hakutufundisha hivyo. Sijui unafanya hivyo kwa kumkumbuka nani??
Migogoro na migongano ya kazini

Wazee wetu walitufundisha wakisema, migogoro na migongano ya kazini ni ukosefu wa nidhamu. Kuna nyakati tunashindwa kuwa watumishi wema wa watu kwa sababu ya migogoro na migongano ya daima, inayojengwa katika ajenda binafsi. Kutokana na migogoro na migongano hiyo, watumishi wengi tunakuwa wenye hasira na "sura ndefu kazini", kiasi kwamba wakija watu kutaka huduma wanayostahili, wanaambulia matusi, lugha korofi na huduma za kuparazaparaza. Kila mmoja ajitahidi sana kujenga amani katika maeneo ya kazi, ili tuwezeshane kuwahudumia watu vizuri.

Utashangaa muda mwingi wa kazi tunatumia kwa ajili ya vikao vya kusulihisha wafanyakazi wakarofi, wavivu, wapiga majungu na wazushi. Katika hili kanuni ni mmoja, tukitaka kufanya kazi vizuri, tutenganishe kati ya tabia zetu na wajibu. Tunapopaswa kutekeleza wajibu na tufanye hivyo. Usilete tabia za nyumbani kwako au za ukoo wako mahali pa kazi. Utaleta harufu mbaya mahali pa utumishi.

Kugubikwa na mitaala ya kishetani

Hili ni jambo linaloitesa sana jamii yetu ya sasa. Wengi tumeingiliwa sana na mitaala ya kishetani na imani kwa nguvu za giza. Hilo lipo kwa wote, wasomi na wasio wasomi. Dhana kama hizo zikijengeka mahali pa kazi, watumishi tutashindwa hata kupeana mikono, tutashindwa kuwahudumia watu vizuri. Na wapo wenye bahati mbaya kubwa zaidi, wale ambao ni waamini haswa wa ushetani na wamemvaa na kumnywa shetani na tabia zake zote. Matokeo yake wanakuwa na virusi vya vurugu kila wakati. Akija kazini tu, amani imetoweka, wenzake hawasalimiani, vitu vinapoteapotea nk. Kumbe ni shetani ndiyo anafanya kazi ndani mwake.

Shetani hakupi chochote zaidi ya kiburi, hofu, ukorofi na kila aina ya uharibifu. Tufanye nini basi? Katika hili, tuimarishe imani yetu kwa Mungu, tusimame imara katika imani yetu, tufanye kazi kwa jina la Mungu, kwa nguvu ya Mungu na katika uwepo wake. Hapo kweli tutaweza kuwatumikia watu kama alivyotufundisha Yesu. Mashindano, ubishi, kujiona bora kuliko wengine, hakuna tija kazini. Neno la Mungu linatuimarisha likisema

Mwishoni mwa ainisho hili, kila mmoja ajiulize katika Ukristo wake, ‘hayo unayoyatenda na hivyo unavyotenda, ni kwa mfano wa nani? Yanamtangaza Kristo kweli?

Katika somo lilopita, na somo hili la leo, tunajaribu kujiweka sawa maisha yetu ya kipasaka yaweje. Tumeona kwamba ili kweli tuwe watu wa Kipasaka, waliotoka makaburini, wanajibudisha kutorudi tena makaburini, ni vema tuishi maisha ya kiekaristi, maisha ya kujimenga na kujisadaka kwa ajili ya wengine, na maisha ya utumishi mwema, utumishi mnyenyekevu kwa wengine. Ni kwa njia hiyo tu maisha yetu mazima yatakuwa ni ukumbusho wa uwepo wa Yesu mwenyewe kati ya wanadamu.

Tunamwomba Kristo Bwana aliyependa kuwa kielelezo kwetu, kielelezo cha Utumishi mnyenyekevu, atupe nguu ya kupenda aliyopenda yeye, kutumikia alivotumikia yeye, ili mwisho wa hija yetu, sote tukastahili kupata tuzo la mtumishi mwema na mwaminifu. Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.







All the contents on this site are copyrighted ©.