2014-05-25 09:48:04

Umefika wakati wa kuchukua maamuzi magumu kwa ajili ya kudumisha amani na utulivu!


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 25 Mei 2014 majira ya asubuhi amehitimisha hija yake ya kichungaji nchini Yordan na kuagwa na viongozi wa Serikali na Kanisa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Malkia Alia, mjini Amman na kuanza safari ya kuelekea Bethlehemu. Alipowasili Uwanja wa Ndege wa Bethlehemu, Baba Mtakatifu amepokelewa na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Palestina na moja kwa moja akaelekea Ikulu ya Palestina ambako amepokewa na Rais Mahmoud Abbas, akakagua gwaride la heshima na kupata utambulisho wa wajumbe waliokuwa kwenye msafara wake!

Baba Mtakatifu majira ya saa 4:00 kwa Saa za Palestina, amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya Palestina. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amegusia matatizo makubwa yanayoendelea kujitokeza huko Mashariki ya Kati na kuwataka viongozi wa Palestina na Israeli kuwa na ujasiri wa kuendeleza mchakato wa amani inayojikita katika haki, usalama pamoja na kutambua uwepo wa Serikali mbili kadiri ya mipaka inayotambulika kimataifa.

Baba Mtakatifu anasema haya ni mambo msingi katika harakati za kukabiliana na hatimaye kusuluhisha matatizo mengine, ili hatimaye, waweze kupata uwiano mzuri wa maendeleo na mfano wa kuigwa na mataifa mengine yanayokabiliana na kinzani kama hizi.

Baba Mtakatifu amegusia mchango mkubwa unaotolewa na Jumuiya ya Kikristo katika mchakato wa maendeleo endelevu na mafao ya wengi. Wakristo wanapenda kuendelea kuchangia katika mikakati ya maendeleo kama raia wengine, wakiwa na haki sawa na kutambuana kama ndugu.

Baba Mtakatifu anashukuru uhusiano mwema uliopo kati ya Palestina na Vatican na kwamba, wanaendelea kufanya maboresho katika Itifaki ya ushirikiano kati ya pande hizi mbili mintarafu Jumuiya ya Wakatoliki nchini Palestina, kwa kukazia uhuru wa kidini, nguzo muhimu katika ujenzi wa amani, udugu na utulivu.

Papa anasema, huu unaweza kuwa ni mfano bora wa kuigwa duniani kwamba, kuna uwezekano wa watu wenye imani, dini na tamaduni tofauti wakaishi kwa pamoja bila kinzani, kwa kutambua kwamba, wana mambo mengi yanayowaunganisha, hivyo ni wajibu wao kutafuta sera na mikakati itakayowawezesha kuishi kwa amani na utulivu; kwa kuzingatia sheria, tofauti zinazojitokeza, lakini wote wakitambuana kwamba, ni watoto wa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi wa Palestina kwa mapokezi makubwa waliyomkirimia. Anasema, mgogoro wa vita unaoendelea huko Mashariki ya Kati kwa miaka mingi umekuwa ni chanzo cha mateso makubwa ya watu, kiasi kwamba, kuna wasi wasi mkubwa wa usalama wa watu na mali zao; kutoheshimiwa kwa haki msingi za binadamu, ubaguzi, makundi makubwa ya wakimbizi, migawanyiko na mahangaiko ya watu. Umefika wakati wa kumaliza migogoro hii, kwa ajili ya mafao ya wengi, changamoto ya kuongeza nguvu katika kutafuta amani kwa kuheshimiana pamoja na kudumisha usalama wa raia.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, viongozi wa Palestina na Israeli wataweza kuanzisha mchakato wa amani kwa ajili ya mafao ya wengi.







All the contents on this site are copyrighted ©.