Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican ambaye yuko kwenye msafara wa Baba
Mtakatifu Francisko Nchi Takatifu anasema kwamba, Papa Francisko alipomaliza kuzungumza
na viongozi wakuu wa Serikali ya Palestina, mjini Bethlehemu, wakati akielekea kwenye
Uwanja wa Pango la Mtoto Yesu kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, ameshuka
kwenye gari na kusali kwa kitambo kidogo kwenye ukuta unaotenganisha Bethlehemu na
Israeli.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa chakula cha mchana kilichoandaliwa
kwa ajili yake, wameshiriki pia Familia za wananchi wa Palestina pamoja na wakimbizi.
Baada ya mapumziko mafupi, Baba Mtakatifu alikwenda kutembelea Kanisa kuu la kuzaliwa
kwa Bwana mjini Bethlehemu.
Majira ya jioni, Baba Mtakatifu ametembelea Kituo
cha "Phoenix Centre" kinachotoa huduma za kijamii ndani ya Kambi ya wakimbizi. Kituo
hiki kilibahatika kutembelewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000. Ujenzi
wa kituo hiki ni ufadhili wa Mtakatifu Yohane Paulo II na kilifunguliwa wakati wa
Jubilee ya miaka 25 ya Utume wa Yohane Paulo II kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baba
Mtakatifu Francisko amepata fursa ya kuonana na kusalimiana na watoto wanaotunzwa
kituoni hapo pamoja na kusali nao na baadaye, Baba Mtakatifu Francisko alihitimisha
hija yake ya kichungaji nchini Palestina na kuagwa kuelekea Israeli ambako amepokelewa
rasmi kwenye Uwanja wa Ndege wa Ben Gourion ulioko Tele Aviv. Amekagua gwaride la
heshima pamoja na kutoa hotuba yake ya kwanza nchini Israeli.