Jimbo kuu la Dar es Salaam lazindua Mwaka wa Familia
Jumamosi ya tarehe 24 Mei 2014, umati wa waamini zaidi ya elfu kumi wa Jimbo Kuu la
Dar es Salaam, walishiriki katika adhimisho la kufungua Mwaka wa Familia. Adhimisho
hili lilifanyika katika Kituo cha Hija Pugu. Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam,
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ndiye aliyeongoza adhimisho hili, akisaidiwa na
maaskofu wasaidizi: Eusebius Nzigilwa na Titus Mdoe, pamoja na mapadri na mashemasi
kadhaa. Tukio hili liliandaliwa na Umoja wa Wanaume Wakatoliki (UWAKA).
Katika
homilia yake, Mwadhama alisisitiza umoja katika familia, kwani si baba au mama ama
mtoto anayeweza kufanikisha malengo ya familia, isipokuwa ushirikiano wa wao wote.
Usikivu kwa sauti ya Mungu na utii kwa sauti hii ndani ya familia ni kitu cha muhimu
sana katika kukuza tunu za kifamilia. Wanafamilia walionywa juu ya mashindano ya kutaka
kujinufaisha wenyewe, kwani ubinafsi ni sumu ya upendo wa familia.
Mwadhama,
alimuweka mbele ya waamini Mtakatifu Yosefu ambaye ni msimamizi wa Jimbo, kuwa kioo
cha familia zetu. Mt. Yosefu alikuwa msikivu na alijitoa kwa familia yake. Waamini
walipewa changamoto, hasa akina baba, kama Mt. Yosefu angemkana mtoto Yesu, kuwa si
wa kwake, Je, ukombozi wetu ungekuwa wapi? Vivyo, hivyo, kusiwe na maelekeo haya katika
familia zetu, kukataa au kuwabagua baadhi ya watoto.
Mtakatifu huu, alifafanuliwa
zaidi, kwa kuelezewa kuwa ni mtakatifu mkimya akuna mfano wake, hatusikii neno lolote
toka mdomoni mwake. Lakini matendo yake yamewezesha ukombozi wa wanadamu wote kutimia.
Katika maisha yake, hakuwa mbinafsi, hata alipofariki na kuwaacha Maria na Yesu, hakuwaacha
katika hali ya masikitiko au kusambaratika kutokana na ubinafsi wake.
Mwadhama,
aliwasihi waamini, si tu katika ngazi ya familia, lakini hata katika ngazi ya familia
kuu ya jimbo, yale ambayo Familia Takatifu ya Nazarethi imetufundisha tuyaweke katika
matendo yetu ya kila siku.
Adhimisho hili, lilifungamanishwa na matendo mbalimbali,
kuwasha Mshumaa wa Familia, makundi na vyama mbalimbali vya kitume (wanawake, wanaume,
vijana, wastaafu, watoto, Moyo Mtakatifu wa Yesu, Legio Maria na wanakwaya) waliweka
maazimio ambayo watayaishi katika Mwaka huu, hasa kuwa tayari kubadilika na kushiriki
katika uinjilishaji mpya.
Sala ya Mwaka wa Familia ilisaliwa na wanafamilia
wote wa jimbo. Aidha, kulifanyika uzinduzi wa kitabu Mfahamu Mtakatifu Yosefu, ambacho
kinamwelezea Mtakatifu huyu pamoja katika uhusiano aliokuwa nao na wanafamilia takatifu
wa Nazarethi. Mwadhama alikipendekeza kitabu hicho, kiwe mwongozo kwa waamini katika
Mwaka huu.
Matukio mengine ambayo yamepangwa ni uzinduzi wa Mwaka huu katika
kila Parokia mwezi Juni. Aidha, kila familia itapana nafasi kutembelewa na wakleri
ili kubarikiwa na kusimikwa kwa Msalaba na Biblia katika nyumba zao. Kardinali ameomba
makundi matatu mengine yaandae adhimisho ambapo nao kama UWAKA walivyoandaa tukio
hili na kuialika familia nzima, navyo vikundi hivyo vifanye hivyo hivyo. Makundi haya
ni akina mama wakatoliki, watoto na wakreli katika Mwaka huu wa Familia.
Tukio
hili, limekuwa ni mwendelezo mzuri wa Mwaka wa Imani, na waamini wengi baada ya adhimisho
hili, wameonesha kufarijika kwao kwa Kanisa kuzijali na kutaka kuzijengea msingi imara
familia zao.
Na Padre Stefano Kaombe, Jimbo kuu la Dar es Salaam.