2014-05-25 10:08:47

Jengeni madaraja ya haki, amani na uhuru kamili!


Rais Mahmoud Abbas wa Palestina Jumapili tarehe 25 Mei 2014 amemkaribisha kwa mikono miwili Baba Mtakatifu Francisko mjini Bethlehemu mahali apozaliwa Mfalme wa Amani na kwamba, jina la Francisko ni mwaliko wa kuhudumia amani, kulinda na kuwatetea wanyonge na kwamba, Palestina na Vatican ni nchi mbili marafiki.

Anasema, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu katika Nchi Takatifu inapania kuwa ni mfano wa usawa katika haki, wajibu na maridhiano na kwamba, wananchi wa Palestina wanatamani kupata amani ya kudumu. Mchakato wa amani ni mgumu kwani kuna idadi kubwa ya wananchi wa Palestina wamefungwa nchini Israeli, wengi wao kwa sasa wanafanya mgomo wa kususia chakula. Palestina tangu mwaka 1967 inaishi katika mazingira magumu na kwamba, wanaitaka Serikali ya Israeli kuachia mji wa Yerusalemu wazi kwa wote na Palestina iwe huru na Yerusalemu kama mji wake mkuu.

Rais Abbas anasema, bado kuna kuta za chuki na utengano zilizojengwa na Israeli, lakini watu watambue kwamba, wanapaswa kujenga madaraja ya amani, utulivu na uhuru kamili dhidi chuki na kinzani. Palestina inaendelea kujielekeza katika mchakato wa kutafuta amani kwa kushirikiana na Umoja wa Nchi za Kiarabu, pale Israeli itakapoachia maeneo inayoyakalia kwa mabavu. Palestina inatumia fursa hii kutuma ujumbe wa amani na hali ya kuheshimiana, ili kudumisha usalama na mafao ya wengi, kwa kujikita katika haki, ukweli na amani ya kudumu.







All the contents on this site are copyrighted ©.