Kamati ya Mkataba Dhidi ya Ukatil ya Umoja wa Mataifa, CAT imehitimisha kazi ya kupembua
taarifa ya utekelezaji wa itifaki hii kutoka Vatican na kuipongeza kutokana na mabadiliko
makubwa yaliyofanywa na Vatican katika kukabiliana na na ukatili na mambo yote yanayodhalilisha
utu na heshima ya binadamu. Kamati hii imefurahishwa kwa namna ya pekee na majadiliano
katika ukweli na uwazi yaliyooneshwa na ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu.
CAT
INASEMA haijatamka kwamba, Vatican na wadau wake mbali mbali hawajavunja mkataba wa
CAT. Kamati hii inatambua juhudi zilizofanywa na Kanisa, Majimbo na Mashirika ya kitawa
katika mchakato wa kudhibiti nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo Kanisa na
taasisi zake zimewasaidia wahanga wa nyanyaso za kijinsia kwa kuwalipa fidia kiasi
cha dolla za kimarekani billioni 2.5 tangu mwaka 1950 na kwamba, kiasi cha dolla za
kimarekani millioni 78 kimetengwa kwa ajili ya matibabu na huduma nyingine.
CAT
imekataa ushauri wa ujumbe wa Vatican kutafsiri na kuhusisha suala la utoaji mimba
kama unyama na ukatili dhidi ya binadamu, ili kulinda uhuru wa kidini na maoni kuhusu
kulinda na kudumisha maisha ya binadamu. CAT pia imekataa kuhusisha vitendo vya kubaka
na nyanyaso za kijinsia kuhusishwa katika adhabu zinazotolewa na kamati. Ujumbe wa
Vatican umepokea ushauri ambao utafanyiwa kazi kwa wakati muafaka katika utekelezaji
wa Mkataba dhidi ya ukatili wa binadamu.
Akifafanua kuhusu taarifa ya CAT,
Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anasema kwamba, Vatican ilijiunga na itifaki ya mkataba
huu kunako mwaka 2002. Mkutano uliochambua taarifa ya awali kutoka Vatican, ulifanyika
kati ya tehe 5 hadi 6 Mei, 2014. Ifahamike kwamba, Mapadre, kisheria wako chini ya
Maaskofu wao mahalia na kwamba, Kanisa linaendelea kujielekeza zaidi na zaidi katika
kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu kama inavyoonekana katika maisha na
utume wa Baba Mtakatifu Francisko.
Kanisa bado linaendelea kukazia toba na
wongofu wa ndani pamoja na majiundo makini ili kuepuka kashfa za nyanyaso za kijinsia
zilizolikumba Kanisa katika miaka ya hivi karibuni. Kanisa litaendelea kujielekeza
zaidi katika huduma za kichungaji na uinjilishaji mpya kama kielelezo cha uaminifu
kwa Kristo na Kanisa lake!