2014-05-24 16:50:53

Roho Mtakatifu anaandaa, anapaka mafuta na kutuma!


Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Uwanja wa michezo wa kimataifa mjini Amman, nchini Yordan. Hii ni sehemu ambayo iko karibu sana na eneo ambalo Roho Mtakatifu alimshukia Yesu baada ya ubatizo wa toba uliofanywa na Yohane Mbatizaji mtoni Yordan. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amekazia kwa namna ya pekee nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Yesu, kama ilivyo kwa Wakristo kwa nyakati hizi!

Roho Mtakatifu alimshukia Yesu na kumwandaa kwa ajili ya kutekeleza utume wa ukombozi wa mwanadamu. Yesu anaonesha kwamba, ni mtumishi mnyenyekevu na mpole, ambaye yuko tayari kushikamana na binadamu ili kujisadaka bila ya kujibakiza. Hapa ni mahali ambapo Yohane Mbatizaji aliwaandaa watu kuweza kukutana na Yesu Kristo Masiha na hapa Roho Mtakatifu akampaka mafuta kama alivyowapaka Mitume wa Yesu ili waweze kuwa na ari na moyo mkuu kama wa Yesu, ili kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa amani, umoja na mshikamano.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake anasema, Roho Mtakatifu anamtuma Yesu kama Yeye mwenyewe alivyotumwa na Baba yake wa mbinguni na kwamba, Wakristo wote wanatumwa kuwa ni wajumbe na mashahidi wa amani. Roho Mtakatifu anatekeleza mambo makuu matatu: anamwandaa, anampaka mafuta na kumtuma Yesu kutekeleza dhamana yake katika kazi ya ukombozi. Roho Mtakatifu amejionesha katika maisha ya Yesu kwa namna ya pekee tangu alipotungwa mimba tumboni mwa Bikira Maria na kwamba, dhamana yake kubwa imekuwa ni kuwakirimia watu amani na utulivu kwa kutambua kwamba, hata tofauti zao ni utajiri mkubwa.

Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kuwapenda jirani zao kwa upendo wa kimungu unaojikita katika unyenyekevu, udugu, msamaha na upatanisho. Haya ni mambo msingi katika kukuza na kudumisha amani ya kweli na inayodumu.

Baba Mtakatifu anasema, amani ni zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu anayewasaidia waamini kujenga madaraja ya amani katika maisha yao ya kila siku. Hija ya amani inaweza kufanikiwa ikiwa kama watu wanatambua kwamba, ni sehemu ya familia ya binadamu na kwamba, wote ni watoto wa Baba mmoja, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Roho Mtakatifu kwa kumshukia Yesu Mtoni Yordan alianza mchakato wa kazi ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Anawaandaa mioyo ya watu wenye mawazo, lugha, tamaduni na dini, ili kuwapaka wote hawa mafuta ya huruma yanayoponya madonda ya makosa, hali ya kutoelewana na kinzani mbali mbali. Anawatuma katika hali ya unyenyekevu kutafuta na kudumisha amani.

Baba Mtakatifu amewakumbuka kwa namna ya pekee watoto waliopokea Komunio ya kwanza katika Ibada hii, wazazi, ndugu na jamaa pamoja na wakimbizi wengi kutoka Palestina, Syria na Iraq.







All the contents on this site are copyrighted ©.