2014-05-24 11:39:56

Kuelekea katika Umoja wa Kanisa!


Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, Mwaka 1964 umeacha alama ya kudumu katika historia na maisha ya Kanisa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Hapa Wakristo wamejifunza kusameheana kutokana na makosa ya kihistoria na hivyo kuanza kujifunga kibwebwe kwa ajili ya ujenzi wa misingi ya upatanisho wa kweli!

Papa Francisko anaendeleza mchakato huu kwa imani na matumaini makubwa tangu alipoanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, katika mwangwi wa maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana na kusali pamoja na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu. Hili lilikuwa ni tukio la majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika upendo na ukweli, nguzo kuu na dira katika majadiliano ya kiekumene!

Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox kwa sasa wameanza ukurasa mpya kabisa baada ya Makanisa haya mawili kutembea katika giza la chuki na uhasama wa kihistoria na kuweka pembeni mambo msingi yanayowaunganisha kama Wakristo, yaani: Biblia Takatifu na Mapokeo ya Kanisa.

Makanisa haya yalikuwa yameingiwa na kishawishi cha kujisikia kuwa yanaweza kujitosheleza na kujitegemea pasi ya kuhitaji uwepo na ushirikiano wa Makanisa mengine! Tarehe 5 Januari 1964 ukawa ni mwanzo mpya wa hija ya majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho na majadiliano ya upendo katika ukweli, kiasi cha kuanza kuimarisha ari na moyo wa upendo na heshima kati ya Wakristo! Ya kale yamepita, sasa tugange yaliyopo na yale yajayo anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza.

Tume ya pamoja na majadiliano kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox katika kipindi cha miaka 50 imechapisha nyaraka mbali mbali zinazoyasaidia Makanisa haya mawili kujadiliana pamoja na kukumbuka kwamba, wanapaswa kutekeleza agizo la Kristo, yaani wote wawe wamoja, kauli mbiu inayoongoza hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu. Wakristo hawana njia mbadala bali kuendeleza mchakato wa upatanisho na umoja wa Kanisa kama sehemu ya utekelezaji wa mapenzi ya Kristo kwa wafuasi wake!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, hivi karibuni aliitisha Mtaguso mkuu uliowashirikisha wakuu wa Makanisa ya Kiorthodox yaliyoenea sehemu mbali mbali duniani na kuamua kwamba, kunako Mwaka 2016 uadhimishwe Mtaguso mkuu wa Makanisa ya Kiorthodox Duniani, kielelezo cha umoja na mshikamano kati ya Makanisa ya Kiorthodox ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Papa Francisko amekwisha julishwa kuhusu maadhimisho haya na kuunga mkono juhudi hizi ili kuendeleza majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox. Mkutano kati ya Papa Francisko na Patriaki Bartolomeo wa kwanza, Jumapili jioni mjini Yerusalem utakuwa ni kielelezo cha utashi wa Makanisa kuendeleza hija ya majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika upendo na uaminifu kwa kweli za Kiinjili, mchakato ambao umeanzishwa miaka 50 iliyopita. Umefika wakati wa kushikamana na kushuhudia Ukristo hata katika madhulumu na pale ambapo haki, amani na upendo vinakosekana. Umefika wakati wa kusimama kidete kwa pamoja kulinda na kutetea kazi ya uumbaji anasema Patriki Bartolomeo wa kwanza.

Upatanisho ni changamoto kubwa kwa sasa kuliko hata ilivyokuwa miaka 50 iliyopita na kwamba, Mkutano wake na Papa Francisko ni tukio kubwa la kihistoria, ili kwa pamoja kusonga mbele kwa imani na matumaini ili kukuza na kudumisha msingi wa majadiliano, amani na utulivu, tayari kufuata nyayo za watangulizi wao katika huduma kwa Kristo na Kanisa lake.

Hii ni nafasi ya kuwaalika watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika majadiliano ya kweli za Kiinjili na furaha ya kukutana na Yesu Kristo Mfufuka. Jambo hili linawezekana pale tu Makanisa yatakapofaulu kuganga migawanyiko na tofauti zake za ndani, ili upendo na furaha viweze kukamilika katika maisha ya Wakristo!

Miaka 50 imewafunda wakristo kusameheana na kujipatanisha wao kwa wao, ili umoja na mshikamano viweze kutawala tena kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake. Tarehe 25 Mei 2014 ni tarehe itakayokumbukwa katika maisha na utume wa Kanisa!







All the contents on this site are copyrighted ©.