2014-05-24 12:39:42

Jifungeni kibwebwe kuokoa Nigeria!


Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury, Uingereza ambaye pia ni mkuu wa Kanisa Anglikani duniani, anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuisaidia Nigeria katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Kikundi cha Boko Haram, kiasi cha kutishia maisha na usalama wa wananchi wa Nigeria. Wakati wa maneno upita, sasa umebaki muda wa kutekeleza ahadi kwa vitendo kwani watu wasiokuwa na hatia wanaendelea kupoteza maisha yao nchini Nigeria.

Ili kula sahani moja na Kikundi cha Boko Haram kuna haja ya kushirikiana kwa karibu zaidi na Jeshi la Polisi nchini Nigeria pamoja na kuwajengea wananchi uwezo wa kiuchumi na maisha ya kiroho, ili kupambana na umaskini na mmong'onyoko wa maadili na utu wema. Kitendo cha kuwateka wasichana wa shule kinapaswa kulaaniwa na kushutumiwa na wapenda amani pamoja na Jumuiya ya Kimataifa.

Msaada kutoka nje ya Nigeria ni mgumu na una hatari zake kwani wananchi wengi hawana imani sana na nchi za Magharibi ambazo zilikuwa na makoloni yao Barani Afrika, kwani wakati mwingine nchi hizi zimetenda kadiri ya masilahi yao binafsi. Askofu mkuu Welby anasikitika kuona kwamba, bado watu wengi wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na kikundi cha Boko Haram nchini Nigeria.

Msaada utakaotolewa na Jumuiya ya Kimataifa unapaswa kuonesha unyenyekevu wa hali ya juu katika nchi ambayo watu wake wanateseka licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali vitu na watu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuonesha mshikamano na maskini pamoja na wote wanaoteseka kwa njia ya sala na bila shaka Mwenyezi Mungu, iko siku ataweza pia kusikiliza na kujibu sala zao!

Askofu mkuu Welby anasema, Kikundi cha Boko Haram kina silaha za kisasa na unafadhili mkubwa ambao unakifanya kuwa na jeuri kiasi cha kufanya mashambulizi katika nyumba za Ibada, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu.

Misimamo mikali ya kidini ni kati ya mambo yanayochangia kutoweka kwa amani na utulivu, kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, hata viongozi wa kidini wanashirikishwa katika mchakato wa wa kutafuta amani, ili watu waweze kuheshimiana na kuthaminiana na kuona kwamba, tofauti zao ni utajiri, baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala sijambo linalopaswa kuwatenganisha. Serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kwamba, wananchi na mali zao wanapata ulinzi wa kutosha. Njia mbali mbali za kudhibiti Kikundi cha Boko Haram zinapaswa kutafutwa, ili amani na utulivu viweze kurejea tena nchini Nigeria!







All the contents on this site are copyrighted ©.