2014-05-23 09:50:50

Wakati umefika kwa USA na Cuba kuanzisha mchakato wa majadiliano!


Makanisa wanachama wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC nchini Marekani yamemwandikia Rais Barack Obama wa Marekani barua ya kuiomba Serikali ya Marekani kuanzisha mchakato wa majadiliano na Serikali ya Cuba, ili kufufua uhusiano kati ya nchi hizi mbili ambao umekuwa ukisuasua tangu wakati wa vita baridi!

Barua hii ambayo imeandikwa na kutumwa kwa Rais Obama mwanzoni mwa mwezi Mei, 2014 inaitaka Serikali ya Marekani kuangalia uwezekano wa kuachiliwa kwa baadhi ya wafungwa wanaotumikia kifungo nchini Cuba na Marekani. Mabadiliko ya Sera ya siasa ya mambo ya nchi za nje ya Marekani yatakuwa na mafao makubwa kwa wananchi wa pande hizi mbili katika maendeleo yao kiroho na kimwili, wanasema viongozi wa Makanisa nchini Marekani.

Viongozi wa Makanisa wanaitaka Serikali ya Marekani kuiondoa Cuba kutoka katika orodha ya nchi za kigaidi na hivyo kutoa mwanya kwa wananchi wa Marekani na Cuba kuweza kutembeleana na kushirikiana katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kiroho. Wanatambua kwamba, si rahisi kwa Congress ya Marekani kupiga kura ya kuondoa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Cuba kwa siku za usoni kutokana, kumbe, uhusiano wa kawaida lingekuwa ni jibu muafaka kwa nchi hizi mbili ambazo zimeendelea kupimana nguvu kwa zaidi ya nusu karne sasa!







All the contents on this site are copyrighted ©.