Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 6 ya Kipindi cha Pasaka
Karibuni ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika kipindi cha Liturujia ya Neno la
Mungu, tukiwa tayari Dominika VI ya Kipindi cha Pasaka, ambamo tunasikia na kuona
Bwana mfufuka akihaidi zawadi ya Roho Mtakatifu.
Mpendwa mwana
wa Mungu, katika somo la kwanza (Mdo, 8: 5-8, 14-17) tunakutana na Filipo ambaye yuko
mji wa Samaria akihubiri habari njema huko. Katika mahubiri yake hayo au tuseme kazi
zake za kichungaji atatenda ishara nyingi na mojawapo ya ishara hizi ni watu kunasuliwa
toka pepo wachafu, waliopooza kuponywa na ishara nyingine kama hizo zilengazo kuleta
uhuru katika maisha ya watu.
Kwa hakika watu walifurahi kama mwandishi anavyosema
“ikawa furaha kuu katika mji ule”. Mitume waliposikia kuwa Samaria wamepokea Neno
la Mungu waliwatuma Petro na Yohane ili wawawekee mikono kwa ajili ya kushukiwa na
Roho Mtakatifu, maana walikuwa wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu.
Mpendwa
msikilizaji yafaa kuweka jambo hili katika mazingira yake; yaani tunatambua kwa njia
ya historia yakuwa, kwa miaka 6 hivi baada ya kifo cha Yesu Kristu, hakukuwa na shughuli
yoyote ya kueneza Neno la Mungu nje ya Yerusalemu. Ndiyo kusema Mitume na wafuasi
wengine walikuwa wakipiga kazi yao palepale nyumbani. Ilikuwaje sasa wakaweza kutoka
nje ya mji wao? Sababu mojawapo kuu ni mchanganyiko katika jumuiya yaani Wayunani
na Waebrania.
Pole pole kukawepo madhulumu dhidi ya Wayunani ambao walionekana
kuwa hatari kwa maana walikuwa na mawazo mapya tofauti na ya Waebrania na hivi wakaanza
kutimuka na kuondoka Yerusalemu na kuelekea wengine Siria, wengine Antiokia, wengine
sehemu nyingine za utawala wa Kirumi. Jambo hili lilipamba moto hasa wakati wa madhulumu
ya Shemasi Stefano. Basi wale wote waliotimuka kila walipofika kwa ajili ya maficho
walianza palepale kuhubiri habari njema. Ndiyo kusema tayari Kanisa si tena la Kiebrania
bali kwa ajili ya Mataifa.
Mpendwa msikilizaji wa Neno la Mungu, katika kukimbia
huko ndipo tunakutana na Filipo ambaye alikuwa Myunani kati ya wale mashemasi 7. Huyu
alijikuta huko Samaria alikokimbilia kuepuka kuuawa kama Mt Stefano. Basi akijikuta
huko alianza kuhubiri na kubatiza na mahubiri yake yalijaa Roho wa Mungu.
Kwa
sababu ya kazi njema hiyo taarifa zilipelekwa Yerusalemu na kwa kuwa ni Yerusalemu
ni Mama Kanisa, Mitume waliona ni vema waendeleze umoja kati ya Yerusalemu na Makanisa
mapya na hivi walienda huko wakwawekea mikono wakristu wapya ili washukiwe na Roho
Mtakatifu. Katika hili mtu aweza kuuliza hivi hawakuwa wamempokea Roho Mtakatifu?
Tayari walikuwa naye lakini kwa kuwa katika Kanisa la mwanzo kushuka kwa Roho Mtakatifu
Kuliambatana na ishara mbalimbali kama kunena kwa lugha, kutenda miujiza basi alama
hizi zilikuwa bado kuchukua nafasi yake kwa Wasamaria mpaka walipokwenda Mitume.
Aidha
katika hili Mungu apenda kusema kuwa, jumuiya mpya huzaliwa kwa utume wa Neno lakini
haziwezi kukua pekepeke hata kama zimeanzishwa ni lazima daima zijifungamanishe na
Jumuiya Mama. Lazima kuwepo na umoja kamili na unaoonekana katika jumuiya zote.
Katika
Somo la pili (1Mt Petro 3:15-18) Mtakatifu Petro anawaalika watu kuwa tayari kushuhudia
IMANI kwa upole na hofu kwa yeyote awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yao.
Daima kuweni na dhamiri njema ili uweza kushinda madhulumu yawajiayo pasipo haki.
Ni vema kuteswa kwa sababu ya mapenzi ya Mungu kuliko kutenda mabaya. Mfano wa uvumilivu
ni Kristu aliyeteswa pasipo dhambi ili awaokoe wenye kustahili kuteswa; lakini akahuishwa
na Mungu.
Mpendwa mwana wa Mungu, tunajiuliza kwanini Mt Petro anakuja na mahubiri
kama haya! Anatoa mahubiri haya kuwatia moyo wakristu kwa sababu ya madhulumu ambayo
yalianza wakati huo ambayo kihistoria yatadumu kwa miaka 250 hivi baadaye. Anawaasa
wakristu kujifungamanisha na Kristu Masiha asiyeweza kuwaacha katika taabu yao. Anataka
pia kupenyeza ndani ya Wakristu hali na moyo wa utayari kujibu maswali yanayowajia
wakiulizwa kwanini wanayo matumaini na kipi kinawasukuma kuwa na tumaini hilo?
Ili
kuweza kujibu vema na kwa ufasaha maswali ya wasioamini lazima kuwa na imani thabiti
yaani inayosimikwa katika moyo ikiangazwa na Kristu mwanga wa kweli. Ni lazima kuwa
na sababu na vigezo kwanini unaamini! Na kwa namna hiyo basi utaweza kusuka majibu
yako ya kiimani si kwa hekima yako bali hekima ya kimungu. Njia nyingine mwafaka ni
maisha yako ya nje yanayoambatana na imani yako, kama yako sahihi ni majibu tosha
kwa wasioamini.
Mpendwa msikilizaji, Mtakatifu Petro anasonga mbele na mahubiri
yake akisema mkristu yampasa kuwa na lugha nyololo na tamu, yaani hapaswi kuwa na
lugha chafu au ya matusi au tuseme lugha kali mbele ya awaye yote awe mtesi au awe
anayetaka kujua juu ya imani yetu. Lugha ya mkristu hualika na kukaribisha awaye yote
kwa furaha na utulivu.
Haya yote si mapya bali yametendwa na Bwana mwenyewe
katika utume wake mpaka anapokata roho, lugha yake ni laini na ya msamaha kwa watesi
wake. Mpendwa wanateologia wanaona sehemu hii ya barua ya Mtakatifu Petro kama ndio
mwanzo wa Taalilim msingi inayotafuta kuhakikisha kwamba imani si kinyume na maisha
yetu ya kawaida bali ni zawadi hakika ambayo mwanadamu aweza kuishi akimwelekea Mungu.
Katika
Injili (Yn 14:15-21) tunakutana na Bwana akiweka wajibu wa kuzishika amri zake kama
kipimo cha mapendo kwake. Kisha hilo anahaidi kumpeleka Roho Mtakatifu, Roho wa ukweli,
mwalimu, na msaidizi wa kukaa nasi milele. Pamoja na ahadi hiyo anaona hatari iliyopo
yakwamba ulimwengu haumpokei Roho Mtakatifu, lakini hata hivyo twampokea sisi maana
akaa ndani yetu. Bwana anasonga mbele akisema hawezi kutuacha yatima bali aja kwetu,
cha msingi ni kumpenda naye atatupenda na kujidhihirisha kwetu daima.
Mafundisho
haya ni sehemu ya wosia wakati wa chakula cha jioni kabla ya kuteswa kwake. Mitume
wamekwisha elewa kwamba Bwana ataondoka na hivi wanafadhaika. Bwana akijua hilo anawahaidi
Roho Mtakatifu atakayekaa nao mpaka mwisho wa nyakati.
Mpendwa msikilizaji,
Bwana anaweka sharti la kumpokea Roho Mtakatifu, sharti la upendo kwa Mungu. Sharti
hili ni kuzishika amri za Mungu. Katika hili Bwana atatoa tahadhari akisema, Kwa kuwa
ulimwengu hautaki kuzishika amri za Mungu basi hautaweza kumtambua kamwe Roho wa Mungu.
Ulimwengu anaoutaja Bwana unaweza kufikirika kama ni ulimwengu wa wasioamini,
lakini ataka kumaanisha ile sehemu katika mioyo yetu ambayo bado imejifungamanisha
na uovu, na hivi Roho wa Mungu hawezi kuingia hapo! Hivyo yafaa daima kukagua mioyo
yetu kama kweli bado kuna sehemu kama hiyo. Kwa hakika namna ya kuona hilo ni pale
tunaposhindwa kuwapenda ndugu zetu, ni pale tunaposhindwa kuwa mawakili wa ukweli
katika maisha ya kila siku.
Mpendwa mwana Kanisa, Bwana anahaidi Roho msaidizi,
Roho wa ukweli na mwalimu. Huyu ni kwa ajili ya kuwasaidia Mitume wakati wote wa utume
wao na hasa wakati wa taabu. Ni Yule ambaye atawafanya wawe na furaha na tumaini katika
maisha yao yote. Ndiyo kusema ni kinyume kukutana na mkristu asiye na furaha moyoni
mwake wakati amempokea Roho wa Mungu, aliye Roho mfariji. Mitume na wakristu wa kwanza
hawataogopa matisho toka nje au ndani ya jumuiya yao. Hawatakata tamaa hata wakitenda
dhambi bali watasimama haraka na kuomba TOBA.
Kwa ujio wa Roho wa Mungu, Roho
wa ukweli Kanisa linapata uhakika yakwamba Neno la Mungu kamwe halitaingiliwa na virusi
na kupoteza uhalisia wake. Ndiyo kusema wakristu hata hivi leo watambue Neno na ukweli
ni uleule tangu ulipopandwa na Kristu mwenyewe. Miaka 2000 zaidi ya ukristu yatosha
kuhakikisha jambo hilo, yaani Kanisa limesafiri na wakati fulani kuyumbishwa toka
ndani na nje lakini daima Habari njema na ukweli ni hakika.
Mpendwa msikilizaji
wa Neno la Mungu Roho Mtakatifu hafanyi tu kazi ya kulikinga Kanisa, bali hata ile
ya kuliongoza katika kuelekea au kutafuta ukweli. Roho Mt. huandaa moyo wa mtu aweze
kupokea kwa uhuru kamili ufunuo wa Mungu. Roho Mtakatifu huongoza Kanisa linaposafiri
kupitia nyakati mbalimbali, ili yale ambayo Bwana aliyasema kwa namna bila kuyafunua
katika ukomo wake yaweze kueleweka na Mitume na hivi Kanisa linaweza kutambua kile
alichotaka Bwana kwa wakati ule. Mpendwa mwana wa Mungu, kazi yako daima ni kumwomba
Roho Mtakatifu akuangazie ili uweze kutambua ile kweli ya Bwana na hivi ukapate furaha
ikupelekayo katika uzima wa milele.
Nakutakieni furaha tele katika Dominika
hii ya VI ya Pasaka na Mungu azidi kuwa nawe, nawe ukitekeleza mapenzi yake na hivi
ukiongozwa na Roho mwalimu, Roho wa ukweli na mfariji katika maisha yako yote. Tukutane
tena Dominika ijayo, yaani katika siku-sikukuu ya KUPAA BWANA MBINGUNI. Tumsifu Yesu
Kristu. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.