2014-05-23 07:55:56

Papa Francisko ni mjumbe wa majadiliano ya kiekumene, kidini na amani


Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Nchi Takatifu imesheheni matukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na kidini sanjari na kukoleza maendeleo ya binadamu yanayosimikwa katika misingi ya haki, amani na mshikamano wa kidugu. Hii ni hija ambayo ni mwendelezo wa historia ya Mapapa inayowaunganisha na Nchi Takatifu, chimbuko la Kanisa la Kristo.

Papa Paulo VI aliwashangaza sana Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican alipoamua kutembelea Nchi Takatifu, ili kukutana, kuzungumza na kusali pamoja na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu, kama mwanzo mpya wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kutembelea rasmi Yerusalemu pengine na kuwashangaza walimwengu kwa kupanda ndege kwa mara ya kwanza, mwelekeo mpya katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baada ya miaka thelathini na sita, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea tena Nchi Takatifu katika maadhimisho ya Jubilee kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akatembelea tena huko mwaka 2009. Kumbe, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko inaendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene ulioanzishwa na watangulizi wake, miaka hamsini iliyopita; majadiliano yanayowakutanisha Watakati Petro na Andrea kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.

Ni mkutano kati ya ndugu wawili katika Kristo kwani viongozi mbali mbali wa Makanisa ya Kikristo walioko katika Nchi Takatifu wanatarajiwa kushiriki katika tukio hili la kihistoria, ili kusali kwa pamoja kuzunguka Kaburi la Yesu Kristo Mfufuka, ili wote wawe wamoja! Ni hija inayojikita pia katika kukoleza majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na waamini wa dini mbali mbali wanaoishi katika Nchi Takatifu, ili kwa pamoja waweze kujifunga kibwebwe kutafuta na kudumisha amani, upendo na mshikamano wa kidugu, kwa kutambua kwamba, wote wanaunda Familia moja ya binadamu!

Taarifa kutoka Nchi Takatifu zinaonesha kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wako tayari kumpokea Baba Mtakatifu Francisko anapowatembelea kuanzia Jumamosi tarehe 24 hadi Jumatatu tarehe 26 Mei 2014. Sehemu nyingi zinakamilisha maandalizi ya mwisho mwisho kabla ya Baba Mtakatifu Francisko "ajatinga timu" huko Mashariki ya Kati!







All the contents on this site are copyrighted ©.