2014-05-23 08:16:03

Huduma ya matumaini kwa watu wenye shida!


Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè imepeleka msaada wa kibinadamu nchini Sudan ya Kusini na Korea ya Kaskazini, ili kusaidia kuganga mateso na mahangaiko ya watu katika nchi hizi ambazo zimekumbwa na vita pamoja na majanga asilia. Msaada uliopelekwa Jimboni Rumbek ili kusaidia ujenzi wa shule ya msingi, ili watoto waweze kujengewa matumaini ya kesho iliyo bora zaidi kwa njia ya elimu.

Kutokana na vita inayoendelea Kusini mwa Sudan, watoto wengi wameshindwa kuendelea na masomo yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao, kumbe kwa njia ya elimu, Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè inataka kuwajengea watoto hawa uwezo wa kupambana na mazingira yao. Kanisa linapenda kuwajengea mazingira ya amani, utulivu, upendo na mshikamano kati ya watu kama sehemu ya mchakato wa kuponya madonda ya chuki na kinzani za kivita!

Walengwa wakuu wa msaada huu ni watoto wanaotoka kwenye familia ambazo zimekumbwa na ugonjwa wa Ukoma, hali ambayo inawafanya bado kuendelea kutengwa na Jamii.

Jumuiaya ya Taizè imetuma msaada wa dawa za binadamu Korea ya Kaskazini ili kusaidia kutoa tiba katika Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati hasa kwa ajili ya maskini wasiokuwa na uwezo wa kugharimia matibabu. Huu ni msgikamano wa kidugu ulionzishwa kunako mwaka 1998 na tangu wakati huo, Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè imekuwa ikituma shehena ya dawa nchini Korea ya Kaskazini. Jumuiya hii pia inajielekeza katika masuala ya maisha ya kiroho kwa kuchapisha Biblia Takatifu kwa ajili ya matumizi ya Wakristo nchini China. Hizi zote ni huduma za matumaini kwa wale waliokata tamaa!







All the contents on this site are copyrighted ©.