2014-05-23 09:03:11

Binadamu na utunzaji bora wa mazingira wapewe kipaumbele cha kwanza!


Madhara ya mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuwa ni mzigo mkubwa kwa Serikali mbali mbali duniani kiasi hata cha kuathiri huduma za kiuchumi na kijamii zinazotolewa na Serikali kwa wanachi wake na hivyo, kuchangia kuporomoka kwa lishe, makazi na afya ya binadamu kwa ujumla.

Wataalam wanasema kwamba, mabadiliko ya tabianchi yataendelea kuchangia kwa ongezeko la magonjwa yanayohusiana na na mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwa kama hakutakuwa na sera na mikakati makini inayopania kudhibiti hali hii! Hayo yamesemwa na Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, wakati akitoa hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano wa 67 wa Baraza la Afya Duniani unaofanyika mjini Geneva, kuanzia tarehe 19 hadi 24 Mei 2014.

Kutokana na changamoto zote hizi, kuna haja kwa watu kulinda, kutunza na kudumisha mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi, kwa kutunga na kusimamia sera makini za utunzaji bora wa mazingira kama anavyoendelea kukazia Baba Mtakatifu Francisko.

Athari za mabadiliko ya tabianchi zimeendelea kuwa ni chanzo kikuu kinachosababisha kudidimia kwa shughuli za uchumi, uzalishaji na tija katika sekta ya kilimo; kukua na kuenea kwa jangwa kutokana na ukame wa muda mrefu; uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji kutokana mafuriko hali inayochangia kuenea kwa magonjwa ya mlipuko pamoja na kuongezeka maradufu kwa maafa asilia sehemu mbali mbali duniani.

Askofu mkuu Zimowski anasema kuna haja ya kujenga na kuimarisha mshikamano kati ya Jumuiya ya Kimataifa katika kupambana na hatimaye kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa sasa ni chanjo kikuu cha maafa asilia. Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano mkuu wa 67 wa Shirika la Afya Duniani unalipongeza Shirika la Afya Duniani kwa kubainisha mikakati ya kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kama kielelezo cha mshikamano wa kimataifa, ili kupanga na kutekeleza sera zitakazosaidia kukuza maendeleo endelevu ya binadamu na hivyo kuleta mabadiliko yanayokusudiwa katika medani mbali mbali za maisha.

Askofu mkuu Zimowski anasema, utunzaji wa uhai pamoja na mikakati ya kuendeleza afya bora hususan miongoni mwa watu wanaoishi katika Nchi zinazoendelea duniani ni jambo la msingi katika kudumisha ekolojia katika ngazi mbali mbali pamoja na kupambana na magonjwa kwa kutoa miongozo na huduma makini. Vatican itaendelea kuunga mkono katika utekelezaji wa sera elekezi ili kuwasaidia watu sehemu mbali mbali kupambana na magonjwa ambayo wakati mwingine yanakuwa ni mzigo kwa familia.

Baraza la Kipapa limepongeza juhudi za Shirika la Afya Duniani katika mikakati ya maboresho ya afya ya wanawake wajawazito, lishe kwa watoto wadogo, ustawi na maendeleo yao na kwamba, wananchi wanapaswa kuhusishwa kikamilifu katika utekelezaji wa sera na mikakati hii, ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Mkakati wa wanawake kunyonyesha watoto wao ni jambo linaloungwa mkono kama njia ya kudhibiti magonjwa ya ukosefu wa lishe bora. Sheria ziwawezeshe wanawake kunyonyesha watoto wao hata katika maeneo ya hadhara, pale inapoonekana inafaa. Kumbe, sera na mikakati ya afya haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na utunzaji bora wa mazingira!







All the contents on this site are copyrighted ©.