2014-05-22 11:11:24

Jiungeni na vyama vya kitume ili kuyatakatifuza malimwengu!


Askofu mstaafu Alfred Rotich wa jimbo la Kijeshi nchini Kenya, amewataka waamini kujiunga na vyama vya kitume ndani ya Kanisa, ili kusaidia mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili na matakatifu.

Kwa njia hii waamini wataweza kuimarisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya huduma makini. Kwa waamini waliojiandikisha katika vyama mbali mbali vya kitume wanahamasishwa kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu na wala si kuwa ni wanachama wa majina tu. Vyama vya kitume ni kielelezo makini cha tafakari ya kina kuhusu Fumbo la Umwilisho na kwamba, kujiunga na vyama vya kitume ni jambo la maana linalosaidia kuimarisha imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Waamini walei wasimame kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya Kikristo na utu wema na kwa njia hii watakuwa kweli ni chumvi na mwanga wa dunia ambayo kwa sasa imegeuka kuwa kama tambara bovu! Askofu mtsaafu Rotich ameyasema haya hivi karibuni wakati akizungumza kwenye Nyumba ya Watoto yatima inayomilikiwa na kuendeshwa na Shirika la Masista Fukara kutoka Bergamo wanaotekeleza utume wao Jimbo kuu la Nairobi.

Askofu Rotich amewapongeza Masista hawa kwa kujimega bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia watoto yatima katika maisha, malezi na makuzi yao! Shirika hili lilifika nchini Kenya kunako Mwaka 1998 na kuanzisha Jumuiya yake ya kwanza, Jimbo kuu la Nairobi.







All the contents on this site are copyrighted ©.