2014-05-22 09:02:36

Hija ya Papa Nchi Takatifu ni kielelezo cha mshikamano wa kidugu!


Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema kwamba, kuna ugumu wa kuandika matukio ya Kanisa, ikilinganishwa na masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, kwani mambo ya Kanisa ni hija ya Familia ya Mungu kutaka kukutana na Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu.

Ufanisi na matunda ya hija za kichungaji zinazofanywa na Mapapa zinaweza kupimwa kwa kuwa na mtazamo huu na kwamba, viongozi wote hawa wameshiriki katika mchakato wa hija ya watu wa Mungu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaojikita katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu. Haya ni mambo yanayomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya majadiliano ya kidini na kiekumene, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Kila Papa aliyewahi kutembelea Nchi Takatifu katika kipindi cha miaka 50 iliyopita amekuwa na mchango wake maalum katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, ustawi na na maendeleo ya watu: kiroho na kimwili. Hija ya kichungaji iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika Nchi Takatifu ilikuwa na mwelekeo wa maisha ya kiroho kwa kutafakari Fumbo la Umwilisho, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo.

Kanisa limeendelea kujiimarisha katika majadiliano ya kiekumene tangu baada ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, lengo ni kujenga na kuimarisha: imani, umoja na udugu kati ya Wakristo. Ni mwendelezo wa tafakari ya kina iliyofanywa na Kanisa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Padre Andrea Koprowski, mkurugenzi wa vipindi, Radio Vatican anabainisha kwamba, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko inalenga kufanya tafakari ya kina katika historia ya ukombozi wa mwanadamu kwa kutembelea mahali alipozaliwa Yesu, kiini cha historia ya ukombozi iliyomwilishwa katika mazingira na maisha ya watu. Nchi Takatifu ni chemchemi ya imani na mwanzo wa Jumuiya ya Wakristo, mwendelezo wa Agano Jipya na la Milele linalofumbatwa katika maisha na utume wa Yesu na Kanisa lake.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko ni kielelezo cha mshikamano wa kidugu na wananchi wote wanaoishi huko Mashariki ya Kati kwani anakwenda kuwatembelea kama hujaji wa amani, imani na mapendo, changamoto kwa wananchi kujikita katika mchakato wa upatanisho, ili kuganga madonda ya: vita, chuki na kinzani za kijamii, tayari kusameheana na kujipatanisha; utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza.







All the contents on this site are copyrighted ©.