2014-05-22 12:33:48

Boko Haram yatazamwa kwa makini zaidi ..


Utekaji nyara kikundi cha wasichana ulio fanywa na kikundi cha maasi Kaskazini mwa Nigeria, takriban mwezi mmoja uliopita, umeamusha hisia na utendaji mkali zaidi kwa jumuiya ya kimataifa dhidi ya kikundi hicho, ambacho tangu kuanza maasi hakuna vurugu hata moja iliyofanikisha ushindi katika lengo lake, zaidi ya kuteka nyara wasichana wa shule.

Uchambuzi uliofanywa na Kirk Ross na kunukuliwa na Allafrica , 19 Mei 2014, unasema, utekaji nyara huo umekuwa ni mwanzo wa uchunguzi zaidi kwa yale yaliyokuwa yakipuuzwa kwanza, katika nia za kikundi na matukio mengine ndani ya Nigeria ambayo yanaweza kuchangia, uelewa juu ya kikundi cha Boko Haram, tabia yake na vyanzo vya msaada kwa kikundi hicho.

Mwandishi anataja lengo kuu la Boko Haram, bila shaka ni kupinga elimu ya Magharibi , lakini nia kuu iliyofichika ni kupinga ushawishi wa maisha ya nchi za Magharibi katika eneo la Kaskazini mwa Nigeria. Ingawa jina la rasmi la kikundi hiki cha upinzani ni Jama'atu Ahlis Sunna Lidda'awati wal- Jihad, au "kundi la watu wenye nia kueneza mafundisho ya Mtume na Jihad, kikundi hiki kimetambuliwa kwa jina la' Boko Haram, mara nyingi hutafsiriwa kuwa na maana ya elimu wa Magharibi ni haramu , na hivyo moja kwa moja inaonyesha chuki za kiitikadi dhidi ya watu, taasisi na jumuiya zisizokuwa na Kiislamu.

Wanachama wa kikundi hicho cha Boko Haram, wanaiona elimu ya Magharibi, kama ni udanganyifu na ulaghai, unaotafuta kuzamisha idadi kubwa ya watu katika nguvu za Ulaya na hivyo kudhoofisha maadili ya jadi ya Kaskazini.

Jina Boko Haram, hivyo, linakuwa na maana ya kuwa kinyume na itikadi za Magharibi kwa ujumla. Lakini wasomi katika eneo hilo la Kaskazini mwa Nigeria , wanauita utendaji wa Boko Haram kuwa ni msimamo dhidi ya Mungu na upotoshaji wa maadili ya jadi Kiislam Kaskazini mwa Nigeria. Ni kubadili maana ya haki na mawazo ya Kimungu na kuwa ni utendaji wenye ukatili wa kinyama.
Maandamano ya Waalimu
Walimu nchini Nigeria wamefanya maandamano ya siku moja, kushinikiza serikali kuharakisha juhudi zake za kuwatafuta wasichana waliotekwa nyara na kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Boko Haram kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.
Pia maandanamo yalilenga kupinga mashambulizi ya Boko Haram dhidi ya walimu.
Kiongozi mmoja wa walimu hao aliambia BBC kwamba zaidi ya walimu mia moja sabini wameuawa mwaka huu. Alituhumu maafisa wa serikali kwa kutoongeza juhudi za kuwalinda walimu na badala yake kujihusisha zaidi na siasa.
Wakati huohuo, Marekani imetuma vikosi vyake nchini Chad , nchi ambayo inapakana na Nigeria kama sehemu za juhudi zake kusaidia katika kuwatafuta wasichana waliotekwa nyara.








All the contents on this site are copyrighted ©.