Watoto wanaoishi katika mazinhira hatarishi wakatiwa bima ya afya!
Shirika la Wamissionari Wabenediktini wa Afrika katika Jimbo Katoliki la Mbeya kwa
kushirikiana na Idara ya Caritas na maendeleo Jimbo Katoliki la Mbeya, katika kuonesha
upendo na huruma ya kweli wamewasaidia misaada ya sare na vifaa vya shule, wanafunzi
zaidi ya 50 katika shule mbalimbali jijini Mbeya.
Aidha wametoa wito kwa serikali,
watanzania na wahisani wengine wenye mapenzi mema ndani na nje ya Nchi kuwasaidia
watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu mahitaji muhimu pamoja na kuwawezesha
kiuchumi walezi wao ili waweze kuzingatia masomo na kuendelea vema kitaaluma.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti Bi .Margreth Mwashala ambaye ni msimamizi wa kitengo kinachojishughulisha
na akina mama walea pekee (Single mother) kutoka Shirika la Caritas Mbeya anaelezea
lengo la misaada hiyo kuwa ni kuwawezesha wanawake hao.
Kwa upande wake Brother
Gasper Toke, OSB, kutoka Shirika la Kimisionari la Wabenediktini wa Afrika wanaofanya
uchungaji wao Jimboni Mbeya amesema wameanza kutoa misaada hiyo kwa watoto 50 katika
shule za msingi, Jijini Mbeya, ili kukabiliana na changamoto ya hali ngumu ya maisha
inayoweza kuwatumbukiza tena katika umaskini mkubwa. Watoto hao wamekatiwa Bima ya
Afya, ili waweze kuendelea na masomo yao bila wasi wasi.
Kwa upande wao wanafunzi
waliopokea misaada hiyo Neema Immanuel na Kevin Chaula kwa niaba ya wenzao nao wamelishukuru
shirika la Wabenediktini na Caritas Mbeya na kuiomba jamii iwaangalie kwa jicho la
huruma ili waweze kuhitimu na kuendelea na masomo ya juu zaidi ili kuweza kujijengea
uwezo wa kupambana na mazingira kwa siku za usoni.
Jumla ya watoto 50 kutoka
katika shule za msingi Ikuti,Simike na Nsongi wamepatiwa misaada mbalimbali na shirika
la kimisionari la wabenedikti wa waafrika kwa kushirikiana na Shirika la Caritas Mbeya
kwa kuwakatia bima ya afya ikiwa ni mwendelezo wa misaada wanayoitoa ili kupunguza
makali ya maisha kwa wazazi wao ambao ni walea pekee.