Kama sehemu ya maandalizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko katika nchi
Takatifu inayoongozwa na kauli mbiu, ili wote wawe wamoja, Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican imekuwa ikikuletea tafakari ya sehemu muhimu za historia ya ukombozi wa mwanadamu.
Leo ndani
ya nyumba, tunaye Padre Benno Michael Kikudo kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam anayewahamasisha
Makleri pamoja na waamini kutembelea Nchi Takatifu kwani imesheheni utajiri mkubwa
wa historia na imani ya Kanisa! Anasema kwa kutembelea Nchi Takatifu mwamini atapata
fursa ya kufahamu Jiografia ya Nchi Takatifu na madhari yake, kikolezo muhimu sana
katika kuyafahamu Maandiko Matakatifu.
Katika nchi Takatifu mwamini anapata
fursa ya kugundua unyenyekevu wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa ajili ya ukombozi
wa mwanadamu, katika mambo yote akawa mwanadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Katika
nchi Takatifu waamini wanaweza kujionea mahali alipozaliwa, alipobatizwa, alipokulia,
alipoteswa, kufa na kufufuka. Hapa mwamini anagusa ukuu wa Mungu unaojionesha katika
maisha ya mwanadamu.
Hii ni historia ya Mwenyezi Mungu anayeshirikiana na
binadamu katika kutekeleza historia ya ukombozi. Padre Benno Michael Kikudo ambaye
ametembelea Israeli kwa zaidi ya mara moja anasema, kila wakati anapata changamoto
ya kutaka kurudi tena kuweza kujitajirisha na maeneo yaliyobarikiwa na kutakatifuzwa
kwa uwepo wa Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu.
Kwa kuangalia maeneo ya kihistoria
tangu wakati wa Agano la Kale hadi Agano Jipya utagundua kwamba, kweli Neno la Mungu
li hai na kwamba, kuna haja ya kumfahamu kwa ukaribu zaidi Yesu Kristo, Jiwe kuu la
pembeni!