2014-05-21 13:56:25

Umoja wa Mataifa wamkumbuka Profesa Maathai Wangai


Jumanne katika ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa , kulifanyika hafla ya kumuenzi hayati Profesa Wangari Maathai, kama kumbukumbu ya kupita miaka kumi tangu mwanamke wa kwanza Mwafrika, kupokea tuzo ya heshima ya amani
Mwanahabari Grace Kaneiya ameripoti kwamba, wakati wa hafla hiyo, Naibu mwakilishi wa kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Koki Muli Grinyo alimtaja Profesa Maathai aligusa maisha ya watu mbali mbali na hata kubadili maisha yao.
Naye Mshauri maalum wa katibu mkuu kwa ajili ya ajenda ya baada ya Maazimio ya mwaka 2015, Amina J. Mohammed, alimtaja Profesa Maathai kuwa kielelezo kwa wote waliokutana naye na kwamba sifa zake zitaishi sio tu nchini mwake Kenya lakini hata nje ya Kenya.
Na kwamba wanapojadili ajenda za baada ya malengo ya milenia ya mwaka 2015, katika muono wa kuwezesha maisha yenye hadhi kwa wote, wachukue hatua kwa kufuata amfano wa Profesa Maathai , katika kuwajali watu wote duniani sawia.
Hafla hiyo ilijumuisha uzinduzi wa bamba maalum lililonakshiwa taarifa kuhusu Profesa Maathai na upandaji wa mti mwingine, karibu na ti aliopandwa na Wangari Mathai katika eneo la Umoja wa Mataifa.
Wangari Muta Maathai alizaliwa Kenya 1 April 1940 na kufariki dunia 25 Septemba 2011 . Alikuwa Mkenya Mwanasiasa na mpenzi wa mazingira. Alipata elimu yake katika shule ya Mtakatifu Scholastica Marekani na pia Chuo Kikuu cha Pittsburgh, na Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya.
Katika miaka ya 1970, Maathai alianzisha kikundi cha kujali mazingira kilicho julikana “Green Belt Movement”, kikundi cha kujitegemea katika kujali mazingira, kisicho kuwa cha kiserikali, na kililenga zaidi katika juhudi za upandaji wa miti, uhifadhi wa mazingira, na haki za wanawake. Mwaka 1986, alituzwa tuzo ya Haki ya Maisha, na mwaka 2004, yeye akawa mwanamke wa kwanza Afrika kwa kupokea Tuzo ya Heshima ya Amani kwa mchango wake katika maendeleo endelevu, demokrasia na amani.
Maathai aliwahi kuwa mbunge na naibu waziri wa Mazingira na Maliasili wakati wa serikali ya Rais Mwai Kibaki kati ya Januari 2003 na Novemba 2005. Aidha alikuwa Diwani wa heshima wa Dunia. Mwaka 2011, Maathai alifariki kwa matatizo ya saratani katika mirija ya uzazi.








All the contents on this site are copyrighted ©.