Papa anasali kwa ajili ya China, Bosnia, Erzegovina na Serbia
Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuhitimisha Katekesi
yake, ameelekeza fikira zake kwa wananchi wa Bosnia, Erzegovina na Serbia ambao wameathirika
vibaya kutokana na mafuriko ambayo hadi sasa yamesababisha maafa makubwa kwa maisha
ya watu na mali zao. Hali inaendelea kuwa mbaya zaidi!
Baba Mtakatifu anachukua
fursa hii kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwanza kabisa kujiunga
pamoja naye kwa njia ya sala, ili kuwaombea wote waliofikwa na majanga haya. Ni matumaini
yake kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itajitahidi kutoa msaada wa hali na mali kwa waathirika
wa mafuriko haya.
Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, tarehe 24 Mei
ni Kumbu kumbu ya Bikira Maria Msaada wa wakristo, Kanisa linasali kwa ajili ya kuiombea
China na kwa namna ya pekee, waamini kutoka China watamiminika kwa wingi kwenye Madhabahu
ya Bikira Maria wa Sheshan yaliyoko mjini Shangai kwa ajili ya kusali. Baba Mtakatifu
anawaomba waamini wote kusali ili kwa njia ya maombezi na tunza ya Bikira Maria Msaada
wa Wakristo, Waamini Katoliki nchini China waendelee kuamini, kupenda na kutumainia,
wakijitahidi kudumisha maelewano mazuri na jirani zao.
Baba Mtakatifu anasema,
Jumamosi Ijayo, tarehe 24 Mei 2014, Kanisa litawatangaza Watumishi wa Mungu: Padre
Mario Vergara na Isidori Ngei Ko Lat, Mwamini mlei na Katekista waliouwawa kwa chuki
za kidini huko Birmania kunako mwaka 1950. Ujasiri na uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa
lake viwatie shime Wamissionari lakini zaidi Makatekista ambao wanatekeleza utume
wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa mahalia.