2014-05-21 08:44:27

Kheri na baraka Askofu mkuu Dallu!


Askofu mkuu Damian Dennis Dallu wa Jimbo kuu la Songea amesimikwa rasmi, Jumapili tarehe 18 Mei 2014 katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Mathias Mulumba, Jimbo kuu la Songea na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa waamini kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Songea. Katika Ibada hii, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo Katoliki Bunda kuwa ni msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki Geita.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Damian Dallu amekazia umuhimu wa maadili, malezi na uthabiti katika imani inayomwilishwa katika ushuhuda wa maisha ya waamini. Anasema, ni jukumu la wazazi kuhakikisha kwamba, wanarithisha imani kwa watoto wao, imani ambayo inatolewa ushuhuda katika maisha ya Kanisa dogo la nyumbani, yaani familia.

Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaziishi Amri za Mungu katika maisha yao, kama kielelezo cha kumwilisha imani katika maisha adili. Kwa mwamini anayeshika Amri za Mungu, huyuo ataishi na kutekeleza wajibu wake barabara. Kila mtu atekeleze dhamana yake na wala asiwe ni kikwazo cha maisha na utume wa Kanisa Jimbo kuu la Songea.

Askofu mkuu Dallu akizungumzia kuhusu mchakato wa Katiba unaoendelea nchini Tanzania amewakumbusha watanzania kwamba, kabla ya Katiba kuandikwa kwenye makaratasi, watanzania waliunganika kiroho kwani makaratasi yanaweza kuchakachuliwa wakati wowote. Katiba ya sasa ina mapungufu ambayo yanaweza kurekebishwa, lakini ina mambo mengi msingi yanayowaunganisha watanzania kama taifa moja.

Watanzania wasidhani kwamba, kwa kupata Katiba Mpya matatizo yao yatakuwa yamemalizika, kudhani hivi ni kujidanganya na wala hakuna ukweli ndani yake. Amewataka watanzania kukubali kubadilika na kwamba, Katiba Mpya itoke ndani ya mioyo yao. Ni wajibu wa wajumbe wa Bunge la Katiba kuzingatia maadili bila kupindisha ukweli wa mchakato wa maoni ya Katiba.

Askofu Mkuu Dallu amewataka watanzania kusali ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwajalia kupata viongozi wema na waadilifu watakaowaongoza watanzania kwa kuzingatia msingi ya haki, amani na utulivu, utu na maadili mema, ili Tanzania isitumbukie katika vita na machafuko.



Akizungumza katika Ibada hii, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amewataka waamini wa Jimbo kuu la Songea kumpokea Askofu mkuu Damian Dallu na kumwonesha ushirikiano mkubwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Jimbo kuu la Songea. Amempongeza Askofu mkuu Dallu kukubali uteuzi wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuliongoza Jimbo kuu la Songea.

Askofu Ngalalekumtwa amekemea tabia ya wizi na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kuwa ni matendo yanayomchukiza Mungu na binadamu. Dhamira safi, upendo na wema, upole, ukarimu na rehema ndiyo matunda ya sadaka safi inayompendeza Mwenyezi Mungu.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, akitoa salam kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, amewataka watanzania kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa ili kujiletea maendeleo endelevu badala ya kutegemea Serikali au Kanisa kuwaletea maendeleo, jambo ambalo linaweza kuwafanya kuendelea kutopea katika umaskini.

Naye mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu amesema kwamba, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa Askofu mkuu Damian Dallu ili kuunga mkono mchango wa Kanisa katika kuwaletea watu maendeleo hususan katika sekta ya elimu, afya, maji na kilimo.

Katika maadhimisho haya, Jimbo Katoliki la Geita, limewakilishwa na ujumbe wa waamini 120 walioandamana na Askofu mkuu Damian Dallu kutoka Geita, hadi Jimbo kuu la Songea. Waamini wa Jimbo Katoliki Geita walimuaga Askofu mkuu Dallu hapo tarehe 11 Mei 2014 kwa Ibada ya Misa Takatifu.








All the contents on this site are copyrighted ©.