Mtandao wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Duniani, "Talitha kum", umezindua
kampeni dhidi ya biashara haramu ya binadamu inayoongozwa na kauli mbiu "Cheza kwa
ajili ya maisha, pinga biashara haramu ya binadamu" wakati huu Jumuiya ya Kimataifa
inapojiandaa kwa ajili ya kushuhudia mashindano ya Kombe la Mpira wa Miguu Duniani
yatakayofanyika nchini Brazil kwa mwaka 2014. Biashara haramu ya binadamu inawadhalilisha
watu zaidi ya millioni ishirini sehemu mbali mbali duniani.
Kardinali
Joao Braz de Aviz katika hotuba yake ya ufunguzi amesema kwamba, watawa ni watu wanaotekeleza
utume wao kati ya maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa njia hii
wanagusa kwa mikono mahangaiko na mateso ya mwanadamu hususan kwa wale wanaotumbukizwa
katika biashara haramu ya binadamu, kielelezo cha utumwa mamboleo.
Baba Mtakatifu
Francisko anasema kwamba, biashara haramu ya binadamu ni janga katika maisha ya binadamu
dhidi ya upendo wa Mungu unaokoa na kumkirimia mwanadamu maisha mapya.
Ubalozi
wa Marekani mjini Vatican unaunga mkono pia kampeni hii dhidi ya biashara haramu ya
binadamu na kwamba, Serikali ya Marekani inashirikiana kwa karibu zaidi na Baraza
la Maaskofu Katoliki Marekani ili kuwatambua watu ambao wametumbukizwa katika biashara
hii na hatimaye, kuwapatia msaada wa hali na mali ili kuweza kuanza tena upya maisha!
Shirikisho
la Mashirika ya Watawa wa Kike Kimataifa linasema kwamba, katika utekelezaji wa utume
wake, limekutana na watoto, wasichana na wanawake waliotumbukizwa kwenye biashara
ya ngono na kuuzwa kama bidhaa sehemu mbali mbali za dunia.
Hii inatokana
na ukweli kwamba, biashara haramu ya binadamu inaendelea kuwapatia faida kubwa wahusika.
Takwimu zinaonesha kwamba, faida inayotokana na boashara hii haramu imefikia kiasi
cha dolla za kimarekani billioni 32 na faida hii inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka,
kiasi cha kuanza kuipita biashara haramu ya silaha pamoja na dawa za kulevya.
Mtandao
wa Talitha Kum, ulianzishwa kunako mwaka 2009, hadi sasa unajumuisha wanachama wa
Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kutoka katika nchi 79. Kuna watawa 800 kutoka
katika Mashirika 240 wanaojihusisha na kampeni dhidi ya biashara haramu ya binadamu.
Biashara hii inawahusisha "watu wazito", kumbe kuna haja ya kushirikiana kwa dhati
ili kuwapatia watu matumaini ya maisha mapya.
Mashindano ya Kombe la Mpira
wa Miguu Duniani yaliyofanyika nchini Ujerumani na Afrika ya Kusini yaliwapatia watu
wengi fursa za ajira. Vijana wengi wakachangamkia nafasio hizi kutoka vijijini kuelekea
mijini wakitumaini kupata fursa za ajira, matokeo yake wengi wao wakajikuta wakitumbukizwa
kwenye biashara haramu ya binadamu, utu na heshima yao vikaingia mchanga!
Kampeni
dhidi ya biashara haramu ya binadamu inapania kupiga vita biashara ya ngono ya utalii
wanayofanyishwa watoto na wasichana, kazi za suluba pamoja na biashara haramu ya viungo
vya binadamu. Hapa utu na heshima ya binadamu viko hatarini kutokana na baadhi ya
watu kupenda mali na utajiri wa haraka haraka, Brazil inaongoza katika biashara hii.
Watu wengi wana matumaini ya maisha bora, lakini wanapaswa kuwa macho ili wasije wakatumbukizwa
kwenye biashara haramu ya binadamu na hapo ndoto na matumaini yao, yatafifia na kutoweka
kabisa! Biashara haramu ya binadamu si jambo la kuchezea!