Wafundeni vyema vijana wa kizazi kipya katika maadili!
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Jumuiya ya Ulaya, CCEE, hivi karibuni
limehitimisha mkutano wa wakurugenzi wa shughuli za kichungaji kwenye Vyuo vikuu Barani
Ulaya, mkutano uliokuwa unajadili pamoja na mambo mengine kuhusu umuhimu wa Katekesi
kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu Barani Ulaya, kwa kuongozwa na kauli
mbiu “Nini maana ya kuishi kwa furaha?”.
Wajumbe wamepembua
kwa kina na mapana maisha ya vijana wa kizazi kipya Barani Ulaya na kutoka sehemu
nyingine za dunia. Hili ni kundi la vijana waliozaliwa nyakati za matandao, kiasi
kwamba, ni vigumu kumwona kijana ambaye hana simu ya kiganjani.
Ni vijana
wanaotumia muda wao mwingi kuogelea kwenye mitandao ya kijamii, kiasi kwamba, mahusiano
ya vijana wengi yako kwenye mitandao ya kijamii, kiasi cha kufanya mahusiano ya kawaida
kati ya watu kulega lega. Wazazi na wazee hapo awali ndio waliokuwa na jukumu la kuwafundisha
na kuwafunda watoto wao, lakini leo hii mambo yamebadilika, vijana wamegeuka kuwa
ni waalimu wa wazazi na wazee wao.
Ufahamu umevuka mipaka na wala si jambo
la kupimwa na umri na mang’amuzi ya mtu, bali ni juhudi za mtu katika kutafuta masuala
haya kwenye mitandao. Mwelekeo huu wa maisha umesababisha mabadiliko makubwa katika
utambulisho wa maisha ya vijana ni watu ambao hawana tena rejea kwa wazazi na watu
wazima wanaowazidi umri pamoja na kuwatangulia katika maisha.
Matokeo yake
vijana wa kizazi kipya wanashindwa kuchukua maamuzi magumu katika maisha yao kwa mfano
maisha ya ndoa na familia, kupata watoto ni mambo ambayo hayana kipaumbele cha pekee
kwa sasa na matokeo yake vijana wengi wa kizazi kipya wanakosa uaminifu na udumifu
katika mipango na mikakati ya maisha.
Wajumbe wanasema, kufanya kazi na vijana
wa kizazi kipya kunataka moyo kwani ni kundi linalobadilika kwa mwendo wa kasi kubwa.
Kumbe, ili kuwashirikisha vijana ile Furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo
na Kanisa lake. Injili ina nguvu na uwezo wa kuleta mvuto na mshiko kwa vijana, ikiwa
kama wataandaliwa barabara.
Vijana wajengewe uwezo wa kujisomea na kulitafakari
Neno la Mungu, kwa kutambua kwamba, kwa kumwamini Mungu watakuwa na uhuru wa kweli.
Vijana wasaidiwe kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa
na kwamba, walitafute Kanisa kwa kuhamasishwa na Kristo mwenyewe katika Maandiko Matakatifu.
Vijana wafundishwe kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Vijana wakifundishwa
kutumia vyema mitandao ya kijamii, wanaweza kuwa ni Wainjilishaji wazuri kwa vijana
wenzao katika mitandao ya kijamii. Imani ya Kanisa inaweza kutangazwa kwa kutumia
maneno machache tu na kufikia umati mkubwa wa vijana. Ushuhuda na utakatifu wa maisha
ni nyenzo msingi katika Uinjilishaji Mpya miongoni mwa vijana, hili ni jambo ambalo
linapaswa kutilia mkazo na viongozi wanaojihusisha na utume wa vijana kwenye taasisi
za elimu ya juu na vyuo vikuu. Imeandaliwa na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.