Vatican inazidi kuimarisha sheria na mikakati ya kupambana na uhalifu katika fedha!
Taarifa ya Mamlaka ya Habari za Fedha mjini Vatican, AIF katika taarifa yake kwa Mwaka
2013 inaonesha kwamba, vyombo vya sheria vimeimarishwa kushiriki katika mapambano
dhidi ya makosa ya jinai katika masuala ya fedha. Kumekuwepo na ushirikiano mkubwa
katika uwanja wa kimataifa kiasi kwamba udhidbiti wa Mamlaka ya Fedha umeboreka zaidi.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Vatican, Siku ya Jumatatu tarehe 19 Mei 2014, Bwana Renè
Brulhart, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Habari za Fedha mjini Vatican anasema, tathmini
iliyofanywa na Kamati ya wataalam wa masuala ya fedha kutoka Ulaya, Moneyval, Mwezi
Desemba 2013 kuhusu mikakati iliyochukuliwa ili kudhibiti utakatishaji wa fedha na
ufadhili wa vitendo vya kigaidi, inaonesha kwamba, Mamlaka ina muundo madhubuti katika
kuzuia na kupambana na makosa ya jinai katika masuala ya fedha.
Taarifa ya
mzunguko wa fedha iliyotiliwa mashaka imeongezeka maradufu tangu mwaka 2012 hadi mwaka
2013, hii ni kutokana na weledi, umakini na ufuatiliaji wa masuala ya fedha kwa kushirikiana
na mamlaka mbali mbali. Mamlaka ya Habari za Fedha inaendelea kushirikiana na nchi
pamoja na mamlaka mbali mbali ili kudhibiti uhalifu katika masuala ya fedha. Watu
wanaanza kujenga utamaduni wa ukweli na uwazi kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Mabadiliko
yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika masuala ya fedha kwa nyaraka tatu
muhimu yamesaidia kujenga nguzo kuu mbili kwa ajili ya kusimamia na kupata habari
za masuala ya fedha, ili kuimarisha mikakati ya utawala bora na utekelezaji wa majukumu
kwa kuzingatia kanuni, maadili na weledi. Ukaguzi uliofanywa kwenye Benki ya Vatican,
IOR, unaonesha kwamba, kanuni na sheria zilizowekwa zinaweza kuzuia na kudhibiti utakatishaji
wa fedha na ufadhili kwa vitendo vya kigaidi.