2014-05-20 10:47:32

Majadiliano ya kidini ni muhimu sana!


Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini hapo tarehe 19 Mei 2014 anasema kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kudumisha majadiliano ya kidini ili kujenga amani, umoja, upendo na mshikamano kati ya watu.

Kwa sasa kuna mwelekeo mkubwa kwamba, vita, chokochoko na kinzani sehemu nyingi duniani zinachukua mwelekeo wa kidini, jambo ambalo ni hatari kabisa kwa ustawi na maendeleo ya watu!

Watu wengi anasema Kardinali Tauran wanamhubiri Mungu ambaye anajengeka katika mawazo na muundo wa kibinadamu, kumbe kuna haja ya kuendelea kuhimiza kwamba, binadamu ni viumbe wa mwenyezi Mungu na kwamba, watu wana amini kwa Mungu ambaye ni Muumbaji anayeendelea kuzungumza na binadamu kwa njia ya matukio mbali mbali ya maisha, ili kuonesha ukaribu wake kwa binadamu.

Kardinali Tauran anasema, Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini ni mashahidi wa mchakato wa majadiliano unaofanywa na Mama Kanisa kwa kutambua utajiri mkubwa wa tunu msingi za maisha ya kiroho zilizopatikana katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita. Ni jambo la muhimu kwa Wakristo kujiuliza ikiwa kama majadiliano haya ya kidini yamewasaidia kukua na kukomaa katika maisha yao ya kiroho.

Kardinali Tauran anasema Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI alianzisha mchakato wa majadiliano ya kidini na walimwengu, Mtakatifu Yohane Paulo II akayakita majadiliano katika amani kati ya watu; Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akalielekeza Kanisa kujadiliana na waamini wa dini mbali mbali kwa njia ya upendo katika ukweli na kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko analichangamotisha Kanisa kujielekeza zaidi katika majadiliano ya urafiki unaojikita katika ujasiri, hekima, uvumilivu na udumifu kwa kumtegemea Roho Mtakatifu.

Kardinali Tauran anasema, hata katika zile nyakati ambazo mambo yalikuwa magumu kiasi kwamba, watu kukutana na kujadiliana ilikuwa ni ndoto, lakini bado katika kipindi cha miaka hamsini kumekuwepo na matukio ambayo yameonesha nia ya kutaka kujadiliana, kushirikiana pamoja na kutafuta muafaka kwa yale ambayo yalikuwa yanawatatiza watu.

Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini limekuwa ni msaada mkubwa kwa Makanisa mahalia kukutana na kujadiliana na waamini kutoka katika dini mbali mbali. Baraza hili pia limechapisha hati mbali mbali zinazoweza kulisaidia Kanisa katika mchakato wa majadiliano ya kidini. Ikumbukwe kwamba, majadiliano ya kidini na Uinjilishaji ni chanda na pete kama ilivyo pia katika maisha na utume wa Kanisa.

Padre Miguel Angelo Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini amewashirikisha watu walioshiriki katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Baraza hili kuanzishwa mchango uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika kujenga na kukuza majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani.

Anasema, hii ni sehemu ya mkakati wa ushuhuda wa Injili ya Kristo unaomwilishwa katika matendo, kwa kuwasikiliza waamini wa dini mbali mbali ili kwa pamoja waweze kuishi katika haki, amani, utulivu na udugu. Baraza hili limepitia hatua mbali mbali katika uwepo wake kwa kipindi cha miaka hamsini iliyopita. Viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini katika kipindi cha miaka hamsini wamejikita katika kutembelea waamini wa dini mbali mbali na kufanya nao majadiliano ya kidini; wameandika hati na nyaraka mbali mbali na kubadilishana mawazo.

Mtakatifu Yohane Paulo II kwa mara tatu aliitisha mkutano wa viongozi wakuu wa kidini, ili kukusanyika na kusali pamoja naye mjini Assisi. Kwa mara ya kwanza mkutano huu ulifanyika mwaka 1986, 1993 na mwaka 2002. Viongozi thelathini kutoka katika dini mbali mbali walihudhuria. Tarehe 27 Oktoba 2011 Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliitisha mkutano huu wa sala na kuhudhuriwa na wawakilishi wa dini mbali mbali 180.







All the contents on this site are copyrighted ©.