2014-05-20 06:50:37

Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya wanyonge!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, Baba Mtakatifu hatasita kuzungumza na kukemea pale ambapo amani iko mashakani, kwani hata watangulizi wake, Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II walisimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi, bila kuhofia usalama wa maisha yao, kwani kama viongozi wa Kanisa ni sauti ya kinabii. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu ataendelea kukemea vyanzo vya vita na migogoro ya kijamii inayohatarisha amani na haki msingi za binadamu, mwaliko na changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhu ya migogoro mbali mbali kwa njia ya amani na majadiliano ya kina yanayojikita katika msingi wa ukweli na uwazi, ustawi na maendeleo ya wengi.

Pale itakapobidi, Baba Mtakatifu ataonesha mshikamano wake kwa kutembelea hata maeneo yenye vita na migogoro ya kijamii, ili kuwaonjesha watu umuhimu wa kulinda na kudumisha amani na utulivu.

Kardinali Parolin anasema hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Nchi Takatifu kuanzia tarehe 24 hadi 26 Mei, 2014 ni hija ya amani inayojikita katika majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe wamoja. Ni hija ambayo itamwezesha Baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na viongozi wa kisiasa, katika mwelekeo wa amani.

Migogoro na kinzani huko Mashariki ya kati imekuwa ni chanzo cha mateso na mahangaiko ya watu wengi, mwaliko wa kuachana na falsafa ya mtutu wa bunduki na kuanza kujikita katika majadiliano ya kweli kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Ni matumaini ya Kardinali Parolin kwamba, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko Nchi Takatifu inaweza kuamsha cheche za ujenzi wa msingi wa amani na utulivu, kwani Yerusalem maana yake ni “Mji wa Amani”, lakini kwa bahati mbaya, Yerusalem imekuwa ni kielelezo cha vita na kinzani za kijamii kwa miaka mingi.

Kardinali Pietro Parolin anasema kwamba, ni muhimu sana uwepo wa Umoja wa Mataifa ili kusimamia malengo yake, licha ya mapungufu yanayooneshwa na Umoja wa Mataifa, lakini ni afadhali kwamba, upo, kuliko kutokuwepo kabisa! Umoja wa Mataifa unapaswa kufanyiwa marekebisho makubwa ili uweze kutekeleza majukumu yake katika medani mbali mbali, jambo ambalo halijatekelezwa kwa ufanisi mkubwa licha ya nchi wanachama kuonesha hitaji hili kwa sasa.

Kuna mabadiliko makubwa tangu kumalizika kwa Vita kuu ya Pili ya Dunia, iliyosababisha kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa. Jumuiya ya Kimataifa inahitaji amani endelevu, jambo ambalo limeendelea kuwa ni changamoto kubwa kwa Umoja wa Mataifa, kwani kwa bahati mbaya, dhamana hii anasema Kardinali Parolin imewekwa chini ya usimamizi wa mataifa machache duniani, ambayo wakati mwingine yanatekeleza mafao yao binafsi kwa mgongo wa Umoja wa Mataifa.

Dunia inahitaji Umoja wa Mataifa wenye nguvu, unaosimamiwa na demokrasia ya kweli, hapa Umoja wa Mataifa ungeweza kuwa ni kwa mafao na baraka ya watu wengi zaidi.








All the contents on this site are copyrighted ©.