Jengeni utamaduni wa watu kukutana na kudumisha amani!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 19 Mei 2014 amekutana na kuzungumza na Baraza
la Maaskofu Katoliki Mexico kwa kuwataka kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana
pamoja na kujenga amani. Ili Kanisa liweze kuendelea kuwajengea watu imani na matumaini,
halina budi kushikamana na wahanga wa biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na
maskini!
Baba Mtakatifu anasema, hakuna sababu ya Kanisa kuogopa au kutishwa
na nguvu za giza, bali linapaswa kusimama kidete na kwa ujasiri pamoja na watu wanaoendelea
kuteseka, kwa kutetea haki zao msingi pamoja na kushiriki katika mchakato wa kuwaletea
maendeleo endelevu yanayomlenga mtu mzima: kiroho na kimwili. Mambo haya yanajikita
katika mchakato wa Uinjilishaji pamoja na kutafuta mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu
anasema, Mexico kwa sasa imegubikwa na vitendo vya uhalifu wa kila aina unaowahusisha
vijana, changamoto kwa Kanisa kuanzisha mchakato wa kutafuta na kudumisha misingi
ya haki, amani na utulivu kati ya watu. Hapa kunahitajika utamaduni wa watu kukutana
na kujadiliana kuhusu mustakabali wa nchi yao, ili kwa pamoja waweze kujikita katika
ujenzi wa amani ya kudumu.
Baba Mtakatifu Francisko amegusia kwa namna ya pekee
umuhimu wa waamini waleikushiriki katika maisha na utume wa Kanisa; umuhimu wa majiundo
endelevu ya vijana pamoja na kuwa na mikakati makini inayolinda na kudumisha tunu
msingi za maisha ya ndoa na familia. Waamini wanakumbushwa kwamba, Parokia ni muhimu
sana katika ukuaji wa mtu kiroho na kimwili. Hapa pawe ni mahali pa maisha ya Kisakramenti
na Sala, changamoto ya kujikita katika utume wa familia ili kudumisha Injili ya uhai
dhidi ya utamaduni wa kifo.
Baba Mtakatifu anawaalika Makleri katika ujumla
wao kutojizamisha katika malimwengu kwa kupenda anasa, mali na madaraka, bali daima
wajifunze kwa maneno na matendo yao kuwa ni wafuasi amini wa Yesu Kristo. Maaskofu
wawasaidie watawa kutekeleza dhamana yao katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kujenga
upendo mkalimifu. Wajitahidi kuhamasisha miito mitakatifu na kuitunza kwa ajili ya
ustawi na maendeleo ya Kanisa.