2014-05-20 11:35:40

Amani na utulivu havipatikani katika mali na madaraka!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake Jumanne, tarehe 20 Mei 2014 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican anasema kwamba, mwamini anayempokea Roho Mtakatifu moyoni mwake atapata amani na utulivu wa kweli na wala si katika uchu wa mali na madaraka.

Amani ya kudumu inayozungumziwa na Yesu katika Injili inajionesha kwa njia ya Roho Mtakatifu na kwamba, hii ndiyo kiu kubwa ya binadamu kwa kila nyakati. Kabla ya kujisadaka, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Yesu anawambia mitume wake kwamba, anawapatia amani na wala si kama ile amani inayotolewa na ulimwengu ambayo haina mizizi ndani mwake. Ni amani inayoweza kumkirimia mtu utulivu na furaha kwa kiasi fulani, lakini bado ataendelea kubaki katika utupu!

Baba Mtakatifu anasema, amani na utulivu kamwe haviwezi kupatikana katika mali wala madaraka kwani haya ni mambo ya mpito na yanaweza kuporomoka na hapo mtu akashikwa na bumbuwazi. Waamini wajenge amani na utulivu wao kwa kumtegemea Yesu Kristo, aliyeshangiliwa na Watoto wa Wayahudi, Jumapili ya Matawi na wakamsulubisha Ijumaa kuu, lakini akafufuka siku ya tatu! Yesu ni amani na utulivu wa watu wake!

Amani ni zawadi ya kwanza iliyotolewa na Yesu Kristo mfufuka kwa mitume wake waliokuwa wamejifungia ndani kwa woga na wasi wasi wa Wayahudi. Amani ya Yesu ni zawadi ya Roho Mtakatifu ambayo waamini wanaipokea kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na kuimarishwa kwa katika Sakramenti ya Kipaimara. Katika shida na mahangaiko ya ndani, watu wajitahidi kumkimbilia Roho Mtakatifu, ili aweze kuwakirimia amani na utulivu. Hii ni amani inayotolewa na Mwenyezi Mungu peke yake!







All the contents on this site are copyrighted ©.