2014-05-19 08:49:15

Umuhimu wa familia!


Familia hazina budi kuundiwa mazingira bora ili ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wake katika tamaduni, sheria na uchumi, ili kukidhi mahitaji msingi ya familia pamoja na ukuaji huru wa karama na vipaji vyake. Haya ndiyo mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza katika kongamano la familia kitaifa, lililofanyika mjini Varsavia, Poland, hapo tarehe 17 Mei 2014, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Familia katika Jamii ya kiraia".

Wajumbe wameangalia kwa kina na mapana kuhusu mahusiano kati ya familia na taasisi mbali mbali zinazosimamiwa na Serikali nchini Poland na athari zake. Tema hii ni muhimu sana kwa Kanisa wakati huu linalojiandaa kwa ajili ya Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu itakayofanyika mjini Vatican, Mwezi Oktoba, 2014 na kwa namna ya pekee pia nchini Poland wakati huu wanapojiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu. Wajumbe wamejadili hali ya familia nchini Poland, matatizo, changamoto na fursa zilizopo.

Ili kuunga mkono tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, wajumbe wa kongamano hili wameshiriki katika maandamano ya familia yaliyofanyika kwenye miji mbali mbali nchini Poland.







All the contents on this site are copyrighted ©.