Poland inamkaribisha Papa Francisko kwa mikono miwili mwaka 2016
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 19 Mei 2014 amekutana na kuzungumza na Waziri
mkuu wa Poland Bwana Donald Tusk, ambaye baadaye alikutana na kuzungumza pia na Kardinali
Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Dominique
Mamberti, katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.
Katika
majadiliano ya viongozi hawa wawili wamegusia kwa namna ya pekee tukio la Mama Kanisa
kumtangaza Yohane Paulo II kuwa Mtakatifu na umuhimu wake nchini Poland. Waziri mkuu
Tusk anamkaribisha kwa mikono miwili Baba Mtakatifu Francisko nchini Poland kunako
mwaka 2016 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Viongozi hawa pia wameangalia
hali ya uchumi na kijamii nchini Poland pamoja na kuchambua hali ilivyo katika Jumuiya
ya Kimataifa kwa sasa kwa kuonesha wasi wasi kutokana na kinzani zilizopo Ulaya Mashariki.