Majadiliano ya kidini na kiekumene ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya
Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeanzisha mkakati wa shughuli za kichungaji unaotaka
kuunganisha majadiliano ya kiekumene pamoja na majadiliano ya kidini kama sehemu ya
ushuhuda wa Uinjilishaji mpya unaopaswa kutekelezwa na wanachama wa Baraza la Makanisa
Ulimwenguni katika nchi husika.
Ikumbukwe kwamba, majadiliano ya kiekumene
yanajikita kwa namna ya pekee na Wakristo wa Makanisa mbali mbali wakati ambapo majadiliano
ya kidini yanawahusisha waamini wa dini mbali mbali duniani.
Haya ni maamuzi
yaliyofikiwa hivi karibuni kwenye mkutano wa Tume ya Imani ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni
katika mkutano wake uliofanyika hivi karibuni nchini Uswiss. Wajumbe wameangalia uhusiano,
utofauti na malengo yaliyomo katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini
yanayotekelezwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni.
Wadau wakuu katika majadiliano,
watajengewa uwezo kwa njia ya semina na vitini mbali mbali ili kusaidia mchakato wa
majadiliano ya kiekumene na kidini katika Makanisa mahalia. Mkutano huu uliwashirikisha
wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Kwa mara ya kwanza katika mikakati
yake ya kichungaji, Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaonesha nia ya kuanza kwa kasi
kubwa zaidi majadiliano ya kidini, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani
na utulivu kati ya watu, kwa kuheshimu uhuru wa kuabudu kama ilivyokaziwa wakati wa
maadhimisho ya mkutano mkuu wa kumi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni uliofanyika
mwaka 2013 huko Korea ya Kusini.