2014-05-19 06:52:38

Maisha ya Familia si piknik, yataka kujisadaka kweli kweli! Upo hapo?


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani, tumsifu Yesu Kristo! Karibu kwa mara nyingine tena tutafakari juu ya maisha baada ya Pasaka. Kama tulivyohekimishana katika kipindi kilichopita juu ya wajibu wetu wa kuendelea kujitunza na kubaki katika neema za kipasaka, leo tuendelee kwa kutafakari ni namna gani sasa tuiishi Pasaka yetu. Ni namna gani tumdhihirishe Kristo Yesu katika maisha yetu ya kila siku. RealAudioMP3

Maisha ya baada ya Pasaka ni maisha ya aina gani? Yana sura nyingi sana. Leo tuitafakari moja tu. Maisha ya kipasaka ni maisha ya kiekaristi. Kwa tafakari hii tunataka sisi sote tumtazame Kristo Yesu kama dira ya maisha yetu ya kila siku. Uwepo wake katika Neno na Sakramenti, uyaongoze maisha yetu ya kila siku. Kristo Bwana alipokuja kwetu mara ya kwanza, alipanda mbengu ya ufalme wa Mungu, aliwahubiria watu wokovu, aliponya magonjwa na akamrudishia mwanadamu tumaini la Muungano kamili na Mungu. Aliikamilisha kazi yake hapa duniani kwa kujitoa sadaka mwenyewe kwa ajili ya wokovu wetu.

Matendo makuu mawili yaifafanue tafakari yetu na lengo letu katika mada hii. Tendo la kuweka Ekaristi na kumega mkate (Lk 22:14-20) na tendo la kuwaosha miguu wanafunzi wake (Yoh 13:5-15). Wakati akikaribia kutoa sadaka kuu ya uhai wake kwa ajili yetu sisi aliyotuita rafiki zake, alijiweka Karamuni pamoja na wanafunzi wake. Ni katika karamu ile, Kristo Bwana, alitoa dira ya maisha baada ya Pasaka. Bwana alitwaa mkate, aliubariki, akaumega, akawapa akisema ‘twaeni mle wote, huu ni mwili wangu. Akafanya hivyo na kikombe pia. Mwishoni akaagiza akisema ‘fanyeni hivyo kwa ukumbusho wangu’ (Lk. 22:19).

Walipokuwa bado karamuni, Kristo aliondoka mezani akawaosha miguu wanafunzi wake. Mwishoni mwa tendo hilo-fundishi, Kristo anawauliza swali akisema "Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni? (Yoh 13:12) Basi, ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu, nimewaosha ninyi miguu, nanyi pia mnapaswa kuoshana miguu. (Yoh. 13:14) Na mwisho ansema wazi, “Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni” (Yoh. 13:15). Katika karamu hii na katika tendo hili Bwana anatupatia mfano wa utumishi mnyenyekevu, wa kuhudumiana, kusaidiana. Anatufundisha nasi tuoshane miguu yaani tutumikiane kama yeye alivyotutumikia sisi.

Kwa mwangwi wa matendo hayo ya Yesu, maisha baada ya Pasaka ni vema yawe maisha ya kuhudumiana na kujisadaka kwa ajili ya wengine. Na sasa tuifafanue mada yetu katika uwanja wa Kanisa la Nyumbani, yaani katika familia. Lakini mantiki yake isambae katika maisha mazima ya Mkristo.

Sisi sote tuliofufuka pamoja na Kristo, tunahimizwa sana kuiishi pasaka yetu. Ni kwa njia hiyo tutamfanya Kristo Yesu Mfufuka amwilike katika maisha yetu ya kila siku. Tunaposhiriki mafumbo ya Mungu, tunashiriki nafsi ya Kristo ambaye alikubali kushiriki ubinadamu wetu. Ni kwa njia hiyo na sisi tunakwa siyo tu wabeba Kristo, bali tunaitwa kuwa Kristo mwingine kwa wengine. Sura, uhalisia na utume wa Yesu vionjeke katika maisha ya Mkristo ya kila siku. Kristo hatutamtambulisha kwa majina yetu wala kwa mavazi yetu, wala kwa miujiza ya ajabu, bali kwa matendo ya kawaida maisha yetu ya kila siku.

Tangu tendo la kuzaliwa kwake na hadi kurudi kwa Baba, Kristo alijitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wetu. Katika sadaka hiyo yanafumbwa mambo yoote aliyoyatenda Bwana katika kumkomboa mwanadamu. Na muhutasari wa hayo yote anauweka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya upendo, ambapo yeye anajimega na kujitoa kwa ajili ya wengine. Na anatuagiza akisema fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Maana yake sisi nasi tujimege, tujisadake kwa ukumbusho wa Kristo aliye Bwana na Mwalimu wetu.

Hivyo maisha ya Mkristo baada ya Pasaka, ni maisha ya kujimega, maisha ya kujisadaka. Na hapo ndipo tunapomdhihirisha Kristo kwa ulimwengu, na pia tunaudhihirisha Ukristo wetu. Yeye mwenyewe, alipokuwa akifundisha, akiponya watu, akitetea wanyonge, akikemea maovu, akisali, akiwaombea watu, akihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu na katika yote aliyoyatenda, alikuwa anajimega kwa ajili ya wokovu wetu.

Kwa mantiki hiyo, tuelewe tendo la kujimega kama tendo la kujitoa sadaka katika kuwatumikia wengine. Kujenga hali njema ya wengine. Sisi Wakristo popote tulipo, tunapotenda kazi kwa uadilifu, katika misingi ya utu, imani, haki, na heshima kwa Mungu wetu, hapo ndiyo tunatekeleza neno lile ‘fanyeni hivyo kwa kunikumbuka mimi’.

Sisi Wakristo tunaoshirikishwa Umungu wa Kristo kwa neno na Sakramenti, tunataka kuishi maisha ya kipasaka kwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya huduma zetu adilifu kwa wanadamu wenzetu. Mfano kuhani anapotimiza kazi yake vizuri altareni na katika maisha yake ya huduma ya kikuhani, hapo anajisadaka na kujimega kwa ukumbusho wa Kristo. Mtawa naye anapohudumia watu wa Mungu kadiri ya karama yake, hapo anajisadaka na kummwilisha Kristo.

Askari anapotenda haki katika kazi yake huku akijituma haswa kulinda ufalme wa haki na amani, naye pia anajimega kwa kumkumbuka Kristo. Mwalimu darasani anapofundisha vizuri kwa kujituma kiaminifu, hapo naye anajimega kwa kumkumbuka Kristo. Mhudumu wa afya naye anapohudumia wagonjwa vizuri kwa upendo bila kujihurumia, hapo naye anajimega, anajisadaka kwa kumkumbuka Kristo.

Tusemeje zaidi kwa familia? Watu wa ndoa wana uwanja mpana sana wa kijisadaka, kujitoa kila mmoja kwa mwenzake. Enyi watu wa ndoa, jitoeni sadaka kwa upendo kwa ajili ya wenzi wenu wa agano. Ni kwa njia hiyo tu, furaha na amani itajengeka. Leo ndoa nyingi zinapindapinda kwa sababu wanandoa wengi wamesahau kujitoa sadaka, kujimega kwa ajili ya wenzi wao. Wengi hudhani ndoa ni pikniki na hivyo kufikiria kuwa na maisha ya furaha tuu kama ya mbinguni. Lazima kujijenga katika roho ya kujisadaka kwa ajili ya faida ya wengine.

Huwa inaweza kutokea bahati mbaya mama akafikiri kuwa ni wajibu wa baba peke yake ajitoe, ajimalize, ajisadake kwa ajili ya familia. Au hata baba akawaza kuwa ni kazi ya mama kujisadaka kwa ajili ya familia. Hapo furaha haitajengeka. Furaha hujengeka na kulindwa kwa sadaka.

Wazazi, kuweni wazazi wa Kiekaristi. Ninyi nanyi kwa wito wenu wa ndoa, mmetwaliwa, kwa agano lenu la ndoa mmebarikiwa, ni wajibu wenu sasa kujimega na kujitoa kuhudumia familia zenu. Ni hapo tu, wewe baba, wewe mama utakuwa Kristo mwingine kwa familia yako.

Kuna furaha, faraja na amani tele kama mzazi unajimega, unajisadaka kwa ajili ya familia yako. Kumbukeni neno hili, kuwalea watoto ni msingi-kiapo wa maisha yenu. Siku ile ya agano mliulizwa kama mpo tayari kuwapokea kwa mapendo watoto mtakaopewa na Mungu na kuwalea kama ilivyo sheria ya Kristo na Kanisa lake? Jibu likawa ndiyo!! Iweje sasa mmepewa watoto halafu, msiwatunze, msijimege kwao??

Wanandoa wengi huwa wanajimega na kujimaliza nje ya familia zao. Huko ni kujimega porini, lazima utaambulia maumivu, kuchakaa, kufilisika na mwisho kudharauliwa na kutupwa. Lakini ukijimega katika familia, hiyo ni hazina kubwa sana. Hata kama utaumia sana, hiyo ndiyo sadaka yenye harufu nzuri kwa Bwana. Familia yako itakutuza na kukutunza. Familia yako haitakufukuza kamwe. Ila kule porini unakojimega, sio kwako. Mama, kule porini unakojimega na kujisadaka kwa upendo wote na unafiki mwingi, sio kwako, utazoa uangamizi. Jitoe, jimege, jisadake, jimalize kwa mwenzi wako na familia yako. Hapo utapata heri.

Tunahitimisha kipindi chetu cha leo kwa kukazia neno hili: Sisi tu watu wa kiekaristi, basi na tujitoe kwa ajili ya hali njema ya wengine, ili kristo yesu aendelee kukaa na kung’aa ndani mwetu. Jinsi yeye alivyo sadaka yenye harufu nzuri ya kumpendeza Baba, nasi atayafanya maisha yetu yote yawe ni sadaka nzuri ya kumpendeza Mungu nyakati zote.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.