2014-05-17 12:23:12

Watawa jengeni moyo na ari ya kimissionari!


Askofu Bernadin Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa ambaye pia ni msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki Dodoma amewataka watawa kuonesha ushuhuda wa mashauri ya Kiinjili kwa kujikita katika ufukara, utii na usafi kamili kama kielelezo makini cha majitoleo yao kwa Mungu na jirani katika maisha ya kuwekwa wakfu ndani ya Kanisa.

Watawa wanapaswa kujenga moyo wa usikivu na utii kwa viongozi wao halali, kwa kusali na kutafakari Neno la Mungu linalowawezesha kuisikia sauti ya Mungu ikizungumza kutoka katika undani wa maisha yao! Watambue kwamba, wanaitwa na kutumwa na Kanisa kuwahudumia watu katika medani mbali mbali za maisha, hata kama wakifanya kazi Serikalini wanapaswa kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa na wafanyakazi wengine!

Askofu Mfumbusa ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimbo Katoliki la Dodoma ambapo watawa wanne wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Gemma Galgan waliweka nadhiri zao za daima. Watawa wa Mtakatifu Gemma Galgan na waamini kwa ujumla wao, wanapaswa kujifunza na kuiga maisha ya Mtakatifu Gemma Galgan ambaye ameacha urithi mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Kwa upande wake, Askofu mstaafu Joseph Mathias Isuja wa Jimbo Katoliki Dodoma amewataka watawa kuthamini wito, maisha na utume wao kwa ajili ya Mungu na Kanisa, daima wakijitahidi kujenga na kudumisha fadhila ya uvumilivu, imani, mapendo na matumaini kwa Kristo na Kanisa lake. Watawa wajifunze kuwa ni watu wa sala na Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu kama alivyofanya Mtakatifu Gemma Galgan.

Katika shida na magumu ya maisha, wajitahidi kuyaunganisha na Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, kwani huyu ndiye dira na mwongozo wao wa maisha ndani ya Kanisa. Watawa wajenge na kudumisha moyo wa kimissionari na kitume, tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia!

Na Rodrick Minja,
Dodoma.







All the contents on this site are copyrighted ©.