2014-05-17 09:45:31

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya baada ya mkutano wake wa kawaida wa mwaka uliokuwa unafanyika kwenye Seminari kuu ya Mtakatifu Thoma wa Akwino, Nairobi wametoa tamko linalozungumzia kuhusu kuibuka kwa utamaduni wa kifo nchini Kenya, rushwa na ufisadi pamoja na vita Sudan ya Kusini.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya likizungumzia kuhusu utamaduni wa kifo unaoendelea kushika kasi nchini humo linabainisha kwamba wananchi wengi wanaendelea kupoteza maisha kutokana na mashambulizi ya kigaidi, ajali barabarani, ujambazi, wizi, tabia ya watu kujinyonga kwa kujikatia tamaa, baa la njaa na ulevi wa kupindukia. Hii inatokana na ukweli kwamba, kumekuwepo na silaha za moto zilizozagaa miongoni mwa wananchi wa Kenya, kiasi kwamba, leo Kenya imekuwa ni uwanja wa vitendo vya kigaidi, vinavyoendelea kuwajengea wananchi hofu kubwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaikumbusha Serikali wajibu wake msingi wa kulinda usalama wa raia na mali zao pamoja na wananchi kuonesha ushirikiano wa dhati na vyom bo vya ulinzi na usalama kwani usalama wa nchi uko mikononi mwa raia wenyewe. Ulinzi na usalama vipewe msukumo wa pekee kwani hata askari wenyewe maisha yao yako hatarini, lakini hata hivyo watekeleze wajibu na dhamana yao kwa kuzingatia utawala wa sheria.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema kwamba, rushwa na ufisadi wa mali ya umma kwa sasa ni saratani inayotisha nchini Kenya kutokana na ubinafsi wa kutisha unooneshwa na baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa Serikali. Kumekuwepo na tabia ya ukabila inayoendelea kupandikizwa miongoni mwa wananchi wa Kenya, jambo ambalo ni hatari kwa usalama na maendeleo ya nchi pamoja na vitisho vya mara kwa mara.

Maaskofu wanasema hakutakuwepo na utawala bora, ikiwa kama watu watashindwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuvumiliana na kuheshimiana badala yake wanajikita katika masuala ya kutishiana maisha. Serikali iwe makini na matumizi ya fedha ya umma na kwamba, rushwa na ufisadi ni masuala yanayopaswa kukomeshwa kwa nguvu zote, vinginevyo, wananchi wa Kenya wataendelea kunyonywa!

Rushwa katika Jeshi la Polisi ni chanzo kikuu cha ajali barabarani, changamoto ya kuondokana na vitendo hivi vinavyodhohofisha kanuni na misingi ya utawala bora na badala yake wajikite katika huduma makini kwa ajili ya wananchi wa Kenya. Ni wajibu wa Serikali kukomesha mahusiano yaliyoko kati ya rushwa, biashara haramu ya silaha na wakimbizi; pia kuna uhusiano mkubwa kati ya ongezeko la hali ya umaskini, ukosefu wa fursa za ajira pamoja na ongezeko la vitendo vya wizi na ujambazi nchini Kenya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika tamko lake kwa vyombo vya habari linasema kwamba, maskini ndio wanaobebeshwa mzigo wa ukosefu wa amani na utulivu. Vita inayoendelea Kusini mwa Sudan ni jambo linalokera sana na kwamba, Bara la Afrika haliwezi kuyafumbia macho mateso na mahangaiko ya wananchi wa Sudan ya Kusini! Raia wengi wasiokuwa na hatia wamepoteza maisha yao na wengine wengi wanaendelea kukimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao.

Bara la Afrika bado lina kumbu kumbu ya mauaji ya kimbari yaliyofanyika nchini Rwanda, miaka ishirini iliyopita! Maaskofu wanasema, wasingelipenda kuona maafa haya yanatendeka tena Barani Afrika. Baraza la Maaskofu linachukua fursa hii kuonesha mshikamano wake wa dhati na wananchi wa Sudan ya Kusini katika kipindi hiki kigumu katika historia ya nchi yao.

Kanisa Katoliki nchini Sudan ya Kusini limewekeza sana katika mchakato wa maendeleo endelevu nchini humo. Maaskofu wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa kusaidia harakati za kuwapatanisha wahusika wakuu katika vita Sudan ya Kusini, ili amani iweze kutawala pamoja na kuokoa maisha ya watu wasiokuwa na hatia!







All the contents on this site are copyrighted ©.