2014-05-17 15:59:22

Miaka 50 ya Baraka la Kipapa la Majadiliano ya kidini


Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini lililoanzishwa na Mtumishi wa Mungu Paulo VI kunako tarehe 19 Mei 1964 linaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu lilipozinduliwa rasmi na kuwa ni chombo cha kukuza, kukoleza na kuendeleza majadiliano ya kidini kati ya watu wa mataifa. Mwanzoni kabisa, Papa Paulo VI alianzisha kama Sekretarieti ya majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali, ili waweze pia kupata bahati ya kusikiliza Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa kwao na Mama Kanisa.

Kwa kipindi cha miaka 50, Baraza la Kipapa limesimama kidete katika kuendeleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali, kwa kuyasaidia Makanisa mahalia kutambua dhamana hii kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu katika medani mbali mbali za maisha. Papa Paulo VI alikuwa ni kiongozi aliyeliwezesha Kanisa kufanya majadiliano na ulimwengu. Mtakatifu Yohane Paulo II akalielekeza Kanisa kujikita katika majadiliano ya haki na amani kati ya watu wa mataifa.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linasema, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliliongoza Kanisa kukabiliana na changamoto za majadiliano ya kidini kwa kujielekeza zaidi na zaidi kwenye upendo na katika ukweli. Papa Francisko, kiongozi wa watu anajielekeza zaidi katika majadiliano yanayowawezesha watu kukutana na kujenga utamaduni wa urafiki, umoja na udugu kati yao kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi!







All the contents on this site are copyrighted ©.