Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu imehitimisha kikao chake cha siku mbili kilichofanyika
kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 14 Mei, 2014 ili kupembua muswada wa kwanza wa hati
ya kutendea kazi kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya
familia, "Intrumentum Laboris". Kikao cha kwanza kimehudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko.
Kardinali
Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko
kwa barua aliyomwandika pamoja na kumteua katibu mkuu msaidizi Monsinyo Fabio Fabene
kuwa Askofu, ili kujenga na kuimarisha mshikamano na umoja wa kitume, jambo msingi
na muhimu katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu.
Wajumbe wamepembua kwa
kina na mapana hati ya kutendea kazi na kufanya marekebisho msingi kadiri ya hoja
zilizotolewa. Kanuni mpya za maadhimisho ya Sinodi zimewasilishwa na zitaanza kutumika
hivi karibuni. Mkutano huu wa siku mbili umewahusisha wadau wakuu katika maadhimisho
ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia, itakayoadhimishwa mjini Vatican,
Mwezi Oktoba, 2014.